WAWEKEZAJI wawili katika mashamba ya mifugo wilayani Kilolo mkoani hapa, wametozwa faini ya Sh milioni 10 kila mmoja kwa kulima migomba isiyo rafiki, na mahindi kwenye vyanzo vya maji. Aidha kilimo hicho kimefanyika ndani ya mita 60 za ukingo wa mto Ruaha Mkuu.

Aidha mwekezaji mwingine alikuwa anafanya biashara bila kibali cha Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc). Wawekezaji hao, kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Nemc, Benard Kongola, ni wa shamba la mifugo la Tommy Dairies aliyetuhumiwa kulima migomba na mahindi mita 60 ndani ya eneo la mto Ruaha Mkuu na wa shamba la mifugo la Ndoto, aliyetuhumiwa kufanya biashara bila kuwa na cheti cha tathmini ya mazingira.

Kongola aliwapa wawekezaji hao wiki mbili kuanzia Aprili 24, mwaka huu, wawe wamelipa faini hiyo kwa Nemc, vinginevyo hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa. Pia, alimwamuru mwekezaji wa shamba la Tommy Dairies kung’oa migomba aliyoipanda mara moja ili kuepuka kuendelea kuathiri chanzo cha maji, kwa sababu migomba aliyoipanda ilikuwa si rafiki wa vyanzo vya maji.

Kongola ambaye pia ni Mtaalamu wa sheria katika Kikosi Kazi namba 3 kilichoundwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kurudisha ikolojia ya mto Ruaha Mkuu, alitoa amri ya kung’olewa migomba hiyo na kutoza faini hizo wakati Kikosi Kazi hicho kilipotembelea mashamba hayo hivi karibuni. Katika hatua nyingine, Kongola aliwataka wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji, nje ya mita 60 za maeneo ya vyanzo hivyo kutokubali watu wachache waingize mifugo yao kwenye maeneo hayo au kuendesha kilimo na shughuli nyingine kwa sababu kuwaacha wavitumie hovyo ni uharibifu unaoweza kuvikausha

Tupia Comments: