Kitendo cha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuahidi kutoa tani 500 za mahindi wilayani Longido kimetafsiriwa vingine na Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga.
Ahadi hiyo ya chakula, imetolewa jana na Polepole wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Longido na viongozi wa chama hicho ngazi ya kata na matawi.
Katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe, Polepole amenukuliwa akisema chakula hicho, kitaanza kusambazwa kuanzia Jumatatu na kitauzwa kwa Sh500 hadi 600 kwa kilo.
Hata hivyo, Kalanga alionyesha wasiwasi na kuhoji ni kwa nini chakula hicho kinatolewa Longido? Na kwa nini ni wakati huu?
“Kuna wilaya za Ngorongoro na Monduli zote hizi zina uhaba wa chakula mbona wanapeleka huko pekee?
“Hii ni aina fulani ya ushawishi wa CCM kutaka wakazi wa Longido kuwapa kura, kwa sababu kuna tetesi huenda uchaguzi jimbo hilo ukarudiwa tena,” alisema Kalanga.
Jimbo la Longido awali lilikuwa likiongozwa na Onesmo Ole Nangole (Chadema) lakini uchaguzi ulifutwa.
Tupia Comments: