Balozi wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU), Roeland Van de Geer ameipa Tanzania siri ya kufikia malengo ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

Akizungumza wakati akifunga maonyesho ya wiki ya Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Balozi Van de Geer alisema ili kufikia mafanikio ya viwanda na uchumi wa kati, Tanzania haina budi kuwekeza kwenye na utafiti.

Balozi Van de Geer alisema elimu hiyo inatakiwa kuanza tangu mtoto akiwa mdogo.

Alisema makuzi ya mtoto yanahitaji lishe bora, kumjali, upendo na elimu ya darasani ili baadaye atoe mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Pia, alisema vyuo vikuu vina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, ikiwa vitajikita kwenye utafiti wa kina unaoweza kutoa majibu sahihi ya mahitaji mbalimbali ya jamii.

Balozi huyo aliongeza kuwa EU ipo tayari na itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo elimu na utafiti hasa unaolenga kuibua changamoto za jamii na kutoa suluhisho.

Alisema vyuo hivyo vina mchango mkubwa katika kufikia Tanzania ya viwanda, ikiwa utafiti unaofanywa utalenga kutafuta njia sahihi za kufikia lengo hilo.

“Pia, EU imewekeza kwenye miradi mingi inayofanywa hapa UDSM na nimeipitia nikaona inalenga kutafuta na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya jamii, nachosisitiza ni kwa Tanzania kuendelea kuwekeza kwenye elimu. Mataifa yote hata yaliyoendelea yaliwekeza kwenye elimu,” alisema.

Awali, Mkuu wa Utafiti wa UDSM, Profesa Cathbert Kimambo alisema utafiti mwingi uliofanywa umesaidia katika kutoa suluhisho la maswali magumu, yanayoikabili jamii.

Profesa Kimambo alisema EU ni kati ya wadau wakubwa waliochangia kufanikisha utafiti huo na kwamba, mwaka huu peke yake zaidi ya utafiti 130 umeonyeshwa.

Aliongeza kuwa wameamua kufanya maonyesho hayo ili kuongeza msukumo kwa Serikali na sekta binafsi, kuona haja ya kutumia utafiti katika kufikia uchumi wa viwanda.

Profesa Kimambo alisema matatizo mengi yanayoikabili jamii yanaweza kutatuliwa kwa urahisi kwa kutumia utafiti huo.

Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Profesa Florence Luoga alisema utafiti mwingi uliofanywa chuoni hapo, una uwezo wa kuchangia ukuaji wa maendeleo ikiwa utatumika ipasavyo.

Profesa Luoga alisema kwa muda mrefu chuo hicho kimekuwa kikifanya utafiti mbalimbali, ikiwamo kuzalisha teknolojia rahisi zinazoweza kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya viwanda.

Miongoni mwa utafiti uliowahi kufanywa, ni ugunduzi wa vyura wa kihansi, makaa ya mawe ya mchuchuma, chuma cha liganga, mafuta na gesi.

Tupia Comments: