Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA,, Edward Lowassa asema watumishi 9,932 wa umma wenye vyeti feki inabidi waangaliwe kwa sura ya huruma.
Lowassa aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema anatoa pongezi kwa mambo mengi mazuri yaliyofanywa, lakini katika sakata la vyeti feki, kuwa wapo walioitumikia serikali kwa muda mrefu, na kama wakifukuzwa tu pasipo kulipwa mafao yao basi itakuwa si ubinadamu.
Aidha alizungumzia kuhusu kuzuiliwa kwa kongamano lililokuwa limeandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lililopanga kuwashirikisha viongozi wa vyama vingine ikiwamo Chama cha Mapinduzi na lililolenga kujadili hali ya demokrasia nchini.
Akizungumzia zuio hilo, Lowassa alisema amesikitishwa na kitendo hicho alichodai kimefanywa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tunalaani kitendo hiki kwa lugha inayowezekana, hatua hii ni ya kuminya demokrasia. Nia yetu ilikuwa njema ya kuzungumzia demokrasia. Waandaaji wa kongamano hili waliweka picha yangu na ya Kinana (Abdulrahman KinanaKatibu Mkuu wa CCM) tukionekana tumepeana vichwa lakini tuki smile (tukitabasamu) jambo ambalo ni very important (muhimu),” alisema Lowassa.
Lowassa alisema Tanzania ni moja na watu ni walewale hivyo hakuna tofauti kwa watu wa CCM na Chadema na kwamba kila mmoja kuwa na maoni tofauti hakuna dhambi.
Hata hivyo, Lowassa aliwataka CCM kutambua kuwa ipo siku nchi ya Tanzania itatawaliwa na watu (chama) wengine na siyo wao.
“Kama watashindwa kuondoka wakati wetu, wataondoka wakati wa wajukuu wetu,” alisema.

Tupia Comments: