MAWAZIRI wakuu wastaafu na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Frederick Sumaye pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, leo wanatarajiwa kuongoza waombolezaji kuuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe na Mbunge mstaafu wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kuwepo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, viongozi wa vyama vingine vya siasa, wabunge kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi na wananchi wa kawaida. Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Gulugwa alisema hayo wakati akielezea taratibu zilizopangwa za kuaga zitakazofanyika katika uwanja wa Majengo katika Manispaa ya Moshi.
Alisema mwili utawasili uwanjani hapo leo saa 5:00 asubuhi, ambapo waombolezaji mbalimbali waliomfahamu Ndesamburo watatoa heshima za mwisho na baada ya hapo mwili utarejeshwa nyumbani kwake Mtaa wa KDC, kata ya Kiboriloni, kwa ajili ya kusubiri maziko kesho, Juni 6 mwaka huu.
Ndesamburo alifariki ghafla Mei 31 mwaka huu baada ya kupoteza nguvu za mwili na alifariki akiwa njiani kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi.
Tupia Comments: