Dortmund - Explosion an BVB Bus (Getty Images/M. Hitji)
Polisi ya Ujerumani imemtia mbaroni mwanamme Mjerumani mwenye asili ya Urusi, anayeshukiwa kufanya mashambulizi dhidi ya basi lililokuwa likiwasafirisha wachezaji wa klabu ya Borussia Dortmund wiki iliyopita.
Makomando wa polisi ya Ujerumani, kwa niaba ya ofisi mwendesha mashitaka wa shirikisho wamemkamata mtuhumiwa huyo, mwenye umri wa miaka 28 katika mji wa Tübingen katika jimbo la Kusini Magharibi mwa Ujerumani la Baden Württenberg.
Taarifa za awali kutokana na uchunguzi uliofanywa zimeonyesha kuwa mshambuliaji huyo aliyetambulishwa kwa jina la Sergej W. alitaka kunufaika na kuanguka kwa thamani ya hisa za klabu ya Borussia Dortmund, ambako alitarajia kungetokana na taarifa za mashambulizi kwenye basi iliyobeba wachezaji wa klabu hiyo.
Chanzo ni tamaa ya kutengeneza faida kubwa haraka
Uchunguzi umebainisha kuwa Sergej alikuwa amenunua hisa za klabu hiyo zenye thamani ya euro 78,000 kupitia mtandaoni, akiwa katika hoteli ya klabu hiyo alikokuwa amekodi chumba kuanzia tarehe 9 mwezi huu wa Aprili. Miripuko mitatu ilitokea karibu na basi la Borussia Dortmund siku mbili baadaye, tarehe 11 Aprili wakati wachezaji walipokuwa wakienda kwenye mechi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, dhidi ya timu ya AS Monaco ya Ufaransa.
Screenshot Instagram Marc Bartra 12.4.2017 (Instagram/marcbartra)
Marc Bartra, mchezaji aliyejeruhiwa katika shambulizi hilo
Mchezaji mmoja wa Dortmund, mhispania Marc Bartra alivunjika mkono katika shambulizi hilo, na mechi hiyo iliahirishwa hadi siku iliyofuata. Hali kadhalika, afisa wa polisi aliyekuwa akiendesha pikipiki kusindikiza basi hilo la wachezaji, alipata mfadhaiko kutokana na kelele za miripuko.
Taarifa za uchunguzi zimesema katika ununuzi wa hisa za klabu ya Dortmund, mshukiwa alikuwa amejiwekea uwezekano wa kuziuza tena hisa hizo kwa bei iliyotangazwa kabla, na kulingana na utaratibu wa soko la fedha, kuanguka kwa kiasi kikubwa kwa thamani ya hisa za klabu ya Borussia Dortmund kungempatia faida ambayo ni zaidi ya mara kadhaa ya mtaji aliokuwa ameuwekeza.
Ofisi ya mwendesha mashitaka iliyoitoa ripoti hiyo, imesema iwapo kungetokea vifo vya wachezaji katika shambulizi hilo, thamani ya Dortmund ingeporomoka kwa kiwango kikubwa.
Mashitaka anayokabiliwa nayo mshukiwa huyo ni pamoja na jaribio la kuuwa, kusababisha madhara makubwa ya kimwili kwa wahanga, na pia kusababisha mripuko.
Polisi washukia kuhusika kwa ugaidi
Deutschland Dortmund vor dem Spiel gegen Monaco (DW/C. Ricking)
Polisi walitilia shaka ujumbe ulioachwa eneo la tukio kuashiria kuhusika kwa IS
Awali shambulizi hilo lilikuwa likushukiwa kuwa la kigaidi, kutokana na kikaratasi kilichookotwa eneo la shambulio, kikidai kuandikwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS likikiri kuhusika na miripuko hiyo. Hata hivyo polisi mara moja walitilia shaka ukweli wa ujumbe huo.
Usalama ni suala nyeti nchini Ujerumani wakati huu wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa shirikisho utakaofanyika mwezi Septemba, ambamo azma ya Kansela Angela Merkel kuwania mhula wa nne inakabiliwa na ushindani mkubwa.
Mwaka jana chama cha Bi Merkel kilipoteza uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa, kutokana na sera yake ya kuwafungulia milango wakimbizi zaidi ya milioni moja.
Wasiwasi ulizidi kuongezeka baada ya shambulizi lililofanywa na kijana kutoka Tunisia dhidi ya soko la Krismasi mwaka jana mjini Berlin, ambalo liliuwa watu 12 na kuwajeruhi wengi wengine.

Tupia Comments: