Kenya imekuwa nchi ya kwanza Afrika, kuanza kutoa matibabu bora zaidi kwa watu wanaoishi na virus vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi.
Kwa ushirikiano na serikali ya Kenya, Shirika la kupambana na kifua kikuu, malaria, na HIV/ ukimwi, UNITAD, pamoja na Shirika la Afya Duniani WHO, dawa ya kiwango cha juu isiyotengenezwa na makampuni makubwa ya dawa imetengenezwa ili kuwapatia watu wan chi zinazoendelea.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi habari mjini Nairobi, siku ya Jumatano, Dr Peter Kimuu, mkuu wa idara ya sera za afya na mipango katika wizara ya afya Kenya, alisema dawa hiyo mpya inayojulikana kama Dolutegravir au DTG iliyoidhinishwa Marekani 2013, haina madhara mengi kwa wagonjwa wanoaishi na HIV na haina hatari ya dawa kuwa sugu.
Alisema DTG ni nzuri kwa vile ina madhara madogo sana kulinganisha na dawa nyinginezo.
UNITAID, mshirika wa mpango huo, imetoa karibu chupa laki moja elfu 48 za DTG kwa wizara ya afya ya Kenya ambayo itaweza kuwafikia 1% tu ya watu wanaoishi na HIV.
Robert Matiru, mkurugenzi wa usimamizi wa UNITAID, aliiambia Sauti ya Amerika kwamba faida za kiafya na kiuchumi kutokana na dawa hiyo mpya ni kubwa na kwamba dawa hiyo itaweza kuwa suluhisho la muda mrefu katika kuwahakikisha wagonjwa kupata matibabu wanayohitaji.
"Unapoleta bidhaa ambayo ni rahisi kutengeneza , ambayo ina uwezo mkubwa , hiyo ina maana matokeo mazuri ya matibabu yanapatikana na bila shaka utakuwa unaokoa maisha na fedha, na ni jambo nyeti kwa siku hizi kwani unafahamu ufadhili unapungua na hata kutoweza kupatikana mara nyingine." alisema Dr. Matiru.
Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Kenya, karibu watu milioni moja na nusu wanaishi na HIV nchini humo na kupatikana kwa dawa hii ya kiwango cha juu ni kama kuongeza silaha katika vita dhidi ya janga hili la ukimwi.
Dr. Martin Sirengo, naibu mkurugenzi wa huduma za afya wizara ya afya Kenya alikua na furaha alipokua anazungumza juu ya matibabu hayo mapya. Hata hivyo alisema bado changamoto zipo.
“Tuna changamoto kutokana na kwamba DTG haipatikani kibiashara kuweza kuwapatia kila mtu matibabu. Ni dawa mpya kwa hivyo uzalishaji wake utachukua muda na tunaanza pole pole. Pili matibabu yanabadilika kutoka watu kupewa vidonge vitatu kila siku ambayo ni mchanganyiko usio rahisi hadi kidonge kimoja." alisema Dr. Sirengo
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, zaidi ya watu milioni 18 duniani wanapata dawa za mchanganyiko za ARV. Na DTG inatarajiwa kuanza kutumika katika nchi nyingine mbili za Afrika, Uganda na Nigeria.
Tupia Comments: