WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mpaka sasa jumla ya watumishi wa serikali 2,066 wamehamia Dodoma kutoka Jijini Dar es Salaam.
Ameyasema hayo jana katika viwanja vya Mashujaa mjini Dodoma wakati akifungua maonesho yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Majaliwa alisema azma ya Serikali kuhamia Dodoma ilitangazwa katika viwanja hivyo na Rais John Magufuli.
"Tulitangaza katika viwanja hivi hivi kuwa Serikali itahamia Dodoma na tulisema mpaka ifikapo Februari wafanyakazi wawe wameshahamia sasa ninavyozungumza hapa jumla ya wafanyakazi 2,066 wameshahamia Dodoma,’’alisema Majaliwa.
Amesema kuhamia kwa watumishi hao Dodoma kumeonesha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya tano kuhamisha makao makuu Dodoma.
Majaliwa amesema azma ya serikali ni kuhakikisha inatekeleza yote iliyoahidi kuhusu serikali kuhamia Dodoma.
Pia amesema kuwa Aprili 26 mwaka huu maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakuwa mkoani Dodoma.
Rais Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Majaliwa amesema, maadhimisho hayo ya Muungano yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Jamuhuri mkoani humo.
Aidha Majaliwa amesema pia Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani humo katika uwanja wa Jamhuri.
"Dodoma ndio kila kitu hivyo, sikukuu zote hizo zitafanyikia hapa. Niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi ili tuungane katika kusheherekea sikukuu hizi," amesema.
Tupia Comments: