BAJETI ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imezidi kupaa, baada ya kuomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh trilioni 6.5 katika bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2017/2018.
Kiasi hicho ni takribani asilimia 20.72 ya Bajeti ya Taifa ambayo ni takribani Sh trilioni 31.699. Aidha, kiasi kinachoombwa kimeongezeka kwa Sh 516,240,633,637, sawa na asilimia 8.52 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2016/2017.
Katika fedha zinazoombwa, kumekuwa na ongezeko la Sh 148,397,071,846 katika fedha za miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/2018, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema kati ya fedha zinazoombwa, kiasi cha Sh trilioni 1.78 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo wakati Sh trilioni 4.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Akizungumzia utekelezaji wa bajeti itakayoishia Juni mwaka huu, alisema kumekuwa na mafanikio makubwa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Msingi, Awamu ya Kwanza na ya Pili ambao sasa utekelezaji wake unaingia awamu ya tatu.
Alisema kupitia mpango huo, madarasa ya elimu ya awali zimepatikana shule za msingi 14,946 kati ya shule 16,088 zilizopo, sawa na asilimia 93.33.
Aidha, uandikishaji umeongezeka kutoka 971,716 wa mwaka 2016 hadi kufikia 1,345,636, sawa na ongezeko la asilimia 38.5.
Upande wa uandikishaji wanafunzi darasa la kwanza mwaka huu umefikia 1,842,513 ikilinganishwa na wanafunzi 1,896,584.
Amezungumzia pia kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia, lakini pia utoaji wa posho ya madaraka kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu elimu kata, kuwa kumechangia kuongeza ufaulu kuanzia darasa la nne na kuendelea.
NGUVU BAJETI IJAYO
Alisema kuanzia Julai mwaka huu, Ofisi ya Rais-Tamisemi inatarajiwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini utakaokuwa na jukumu la kufanya tathimini ya mtandao wa barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kusimamia matengenezo ya barabara hizo kila mwaka.
Alisema fedha za utekelezaji wa majukumu ya wakala zitatokana na bajeti ya Mfuko wa Barabara na pia fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Waziri Simbachawene aliongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kupitia Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) na Shirika Lisilo la Kiserikali la Hakikazi Catalyst (HKC), itaelekeza nguvu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Simbachawene, hii italenga kupunguza au kuondoa athari za mabadiliko ya tabia nchi katika mikoa na halmashauri.
Mradi utaanza kutekelezwa kwenye halmashauri 12 zilizoathiriwa zaidi. Kadhalika, itaimarisha pia utoaji wa huduma za afya na lishe ili kupambana na tatizo la utapiamlo alilosema kwa mara ya kwanza mikoa na halmashauri zote nchini zimetenga sh bilioni 11.40 sawa na Sh 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 5 kwa ajili ya huduma ya chanjo na lishe.
Wadau wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali wametenga kiasi cha Sh bilioni 26.48 kwa ajili ya utekelezaji mpango wa kitaifa wa afya za lishe.
WAZEE WAKUMBUKWA
Katika kutekeleza Sera ya kuwapatia tiba bure wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, alisema kufikia Machi mwaka huu wazee 346,889 wametambuliwa na kati yao wazee 74,590 wamepata vitambulisho vya matibabu bila malipo.
Aidha, hospitali za mikoa, wilaya na vituo vya afya vimetenga vyumba maalumu kwa ajili ya huduma za wazee.
Maeneo mengine yaliyoanikwa katika bajeti hiyo ni pamoja na uwezeshaji kiuchumi ukiwalenga zaidi wanawake na vijana.
Imegusa pia usimamizi na uendelezaji vijiji na miji, Mradi wa uimarishaji wa afya ya msingi kwa kuzingatia matokeo, Programu ya kupambana na Ukimwi, Mfuko wa pamoja wa afya, matengenezo na ukarabati wa barabara lakini pia mfumo ulioboreshwa wa kupeleka ruzuku katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGDG) na Mpango wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzania.

Tupia Comments: