SERIKALI imetoa vibali vya ajira mpya kwa nafasi 9,721, na imeahidi kuendelea kuhakikisha utumishi wa umma unaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu.
Kati ya nafasi hizo, vibali 3,174 zimetolewa kwa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza nafasi 1,000, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 8,523 nafasi 297 kwa Uhamiaji na nafasi 50 kwa ajili ya ajira za wataalamu wa afya katika Hospitali ya Kisasa ya Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha, kibali cha ajira kwa nafasi 4,129 za walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati pamoja na nafasi 219 kwa ajira za mafundi sanifu wa maabara za shule vilitolewa na taratibu za ajira kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki alipokuwa anawasilisha makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa Fedha wa 2017/2018 aliyeomba kuidhinishiwa jumla ya Sh 821,322,347,674 (Sh bilioni 831.3).
Kati ya fedha hizo, Sh 390,970,890,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo wakati Sh 430, 351,457,674 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma, itaendelea kusimamia na kuendesha mchakato wa ajira ili kuwezesha waajiri kupata watumishi wenye sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa muundo wa utumishi husika.
Alisema wakati hao wakiombewa ajira, watumishi 19,708 wameondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma kutokana na kustaafu, kuacha kazi, kufariki dunia, kufukuzwa kazi na kumalizika kwa mikataba kwa lengo la kudhibiti watumishi hewa na mishahara batili.
Kuhusu uhakiki wa madai ya malimbikizo ya watumishi, alisema madai 18,823 yenye thamani ya Sh bilioni 32.8 (32,859, 479,490.37) yamehakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mshahara kwa ajili ya malipo.
Aidha, madai ya malimbikizo ya mshahara ya watumishi 12,973 yenye jumla ya Sh bilioni 21.6 (21,615,565,432.71) yanaendelea kuhakikiwa.
Akizungumzia bajeti ya mwaka huu, alisema imezingatia vipaumbele na matakwa ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye kusudio la kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma ili kuondokana na matumizi mabaya ya rasilimali, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na urasimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tunaamini utumishi wa umma uliotukuka ni chachu ya maendeleo kwa taifa lolote duniani, hivyo nasi pia tumejipanga kikamilifu kuhakikisha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake inatoa mchango maridhawa katika kufikia malengo kama taifa na kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Kairuki.
Alisema ofisi yake inaunga mkono kwa dhati juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za kupiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi lakini pia wanaunga mkono hatua stahiki zinazochukuliwa na viongozi katika ngazi mbalimbali ili kurejesha nidhamu na utumishi wa umma na kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tumeanza kuona mafanikio, lakini bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu,” alisema na kuwataka wabunge wenye mapenzi mema kwa nchi kuunga mkono juhudi za serikali.
Akizungumzia Mpango wa Utekelezaji wa mambo muhimu kwa mwaka 2017/18, alisema kwa upande wa Ofisi ya Rais, Ikulu pamoja na mengi mengine imepanga kujenga kuendelea na ujenzi wa Ikulu mpya ya Chamwino, kukarabati Ikulu ndogo za Mwanza, Shinyanga, Mbeya na Moshi.
Kuhusu Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), alisema Serikali inakamilisha uandaaji na utoaji hati za hatimiliki za kimila 11,184 katika halmashauri 14 za Rufiji, Musoma, Sikonge, Chamwino, Kiteto, Meru, Geita, Makete, Kahama, Njombe, Misenyi, Sumbawanga, Misungwi na Magu.
Tupia Comments: