MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amefanya ukaguzi kwenye sekta ya madini na kubaini kuwa mikataba mingi ambayo Serikali imeingia na wawekezaji ina vifungu visivyolinda maslahi ya umma.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa kuna upungufu wa msingi ambao umeonekana katika taratibu zinazotumika kuingia mikataba ikiwemo Serikali kufanya maamuzi kwa kuegemea ripoti ya wawekezaji pamoja na kuwepo kwa vifungu vya kuongeza mikataba ambavyo havina maslahi kwa CAG amebaini kuwa katika majadiliano, Serikali inategemea taarifa za uvumbuzi na upembuzi zilizofanywa na kampuni binafsi inayoomba leseni bila kuwa na njia mbadala ya kuhakiki taarifa hizo hali inayoipunguzia Serikali uwezo wa kutetea maslahi yake.
Katika ripoti yake, alisisitiza kuwa mikataba ya madini iliyopitiwa ilibainika kuwa na vifungu visivyolinda maslahi ya umma kama vile masharti yasiyoridhisha katika kuongeza mikataba.
Alisema kuna vifungu vinavyozuia mabadiliko ya sheria kuathiri mikataba husika, sera zisizoridhisha kwenye fedha za kigeni na forodha, motisha za kodi zilizozidi kwenye taratibu za kihasibu katika kutambua na kutohoa matumizi ya mitaji.
"Serikali inashauriwa itumie kifungu kinachoruhusu kurejewa kwa mikataba kinachopatikana kwenye mikataba mingi ya madini, kinachotumika kurejea makubaliano yaliyoafikiwa na kuhakikisha kuwa Serikali peke yake haiwezi kufanya maamuzi yatakayoathiri matakwa ya wawekezaji kwenye madini ili kuyaita makampuni husika na kujadiliana nayo jinsi ya kuboresha maslahi ya pande zote. "
Vile vile, naishauri Serikali iboreshe usimamizi kwa kampuni binafsi zinazofanya kazi za kutafuta na kuvumbua miamba yenye madini ili kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa sahihi na za ziada zitakazoisaidia kwenye majadiliano na kufanya maamuzi," inasema ripoti hiyo.
Wachimbaji wadogo hawalipi kodi Ripoti inabainisha kuwa licha ya sheria ya usimamizi wa madini kuwataka wamiliki wote wa leseni za kuchimba madini kulipia kodi migodi wanayomiliki na kulipa mrahaba kwa kadri ya uzalishaji wamigodi yao, lakini ukaguzi wa CAG umebaini kuwa, kwa kiasi kikubwa wachimbaji wadogo hawalipi kodi wala mirahaba.
CAG amebaini kuwa kufikia Juni 30, 2016 kuna malimbikizo ya kodi za leseni za migodi inayofikia Sh bilioni 9.8 kutoka kwa wachimbaji wadogo.
Pia amebaini kuwa wachimbaji wadogo wengi hawawasilishi taarifa za uzalishaji wao ili waweze kukadiriwa na kulipa mrahaba na wachache wanaowasilisha.
Pia amebaini kwamba, changamoto hizo zinasababishwa na ukaguzi hafifu kwenye migodi utokanao na uhaba wa fedha, rasilimali watu na kutoa leseni kwa wachimbaji wasio na mitaji na utaalamu wa kuendeleza maeneo yao.
Ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, kuongeza uwezo wa ofisi za madini kanda kwa kuzipatia fedha za kutosha na wafanyakazi ili ziweze kufanya kaguzi za mara kwa mara kwenye migodi ili kufuatilia wachimbaji wadogo wasiolipa kodi za umiliki wa maeneo ya madini na wasioleta taarifa za uzalishaji ili watozwe mrahaba.
Pia ameishauri Serikali iongeze kigezo cha kutathmimi utaalamu na uwezo wa kifedha wa muombaji leseni kabla hajaidhinishwa kupewa leseni.
Migodi yatozwa kodi sifuri
Ripoti hiyo imeeleza kuwa mapitio ya malipo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka kwenye migodi mikubwa minne (4) ya dhahabu Geita, Bulyanhulu, Mara Kaskazini, Pangea na mmoja wa Almasi wa Williamson kwa kipindi cha kati ya Mwaka 2012 mpaka 2016 kulibainika migodi hiyo kurejeshewa kodi kubwa ya VAT ya thamani ya Sh bilioni 1,144.
CAG alisema marejesho hayo makubwa yametokana na mianya inayotolewa na kifungu 55(1) cha sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014, sawia na sheria za zamani ambazo zote kwa pamoja ziliruhusu na bado zinaruhusu tozo ya kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha sifuri kwa bidhaa zinazosafirishwa kuuzwa nje ya nchi.
"Kwa kuwa soko kubwa la madini na vito liko nje ya nchi, madini yote yanayopatikana yanauzwa nje ya nchi na kupelekea kodi inayotokana na manunuzi ya bidhaa za mtaji, mafuta na gharama nyingine yanayofanywa na makampuni ya migodi ndani ya nchi kuzidi ile inayotokana na mauzo," inasema ripoti hiyo.
Alisema kwa hali hiyo, migodi hiyo kustahili marejesho ya kiasi kilichozidi kutokana na kifungu cha 83(2) cha sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014.
Alisema lengo la Serikali kutoza kodi ya ongezekeo la thamani kwa kiwango cha sifuri kwenye bidhaa zote zinazosafirishwa kuuzwa nje ya nchi ilikuwa ni kukuza viwanda vya ndani, mapungufu yaliyojitokeza ni kuwa Sheria hiyo haikuweka makundi kuonesha ni bidhaa zipi zinazostahili motisha hiyo.
"Hivyo basi madini ambayo kwa namna yoyote lazima yauzwe nje ya nchi nayo pia yananufaika na motisha hiyo kama vile ambavyo bidhaa za kilimo na viwandani zinavyonufaika," ilisema ripoti hiyo.
Kwa hali hiyo, CAG ameishauri Serikali kupitia upya sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 na kufanya marekebisho ili kuondoa tozo ya kiwango cha sifuri kwenye mauzo ya madini na vito nje ya nchi.
Alishauri pia Serikali kujadiliana na kampuni ya uchimbaji madini kuhusu matokeo ya mabadiliko hayo kwenye mikataba yao (MDAs).
"Hii ni kinyume na kifungu cha 6 (1) (u) cha sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 inayotaka ushuru wa ndani ulipwe kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mauzo ya mwaka," inasema ripoti ya CAG.
Kutokana na utata huo, CAG ameishauri Serikali kushauriana na kujadiliana na kampuni ya uchimbaji madini kupitia kifungu cha utakaso wa mkataba kinachopatikana kwenye mikataba takribani yote ili kurekebisha viwango vya tozo za kodi kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi vinavyobadilika kufatana na muda tangu kusainiwa kwa mikataba hiyo.
Tupia Comments: