Parachichi ni tunda ambalo mti wake hujulikana kisayansi kama Persea amerikana.  Tunda hili lina aminika kuwa na asili kutoka jimbo la Puebla, bara Amerika ya kusini kunako nchi ya Mexico. Ushahidi wa kale kabisa, takribani miaka 10000 BC umeonyesha parachichi lilitumika katika jimbo la Puebla nchini Mexico. Lakini kutokana na faida nyingi kiafya zipatikanazo kwa ulaji wa tunda hili, tunda hili sasa hupatikana na kutumika kwa lishe sehemu nyingi duniani hususani barani Afrika.

Parachichi ni tunda la pekee ukilinganisha na matunda mengine, kimsingi matunda mengine huwa yana wanga(carbohydrate) kwa wingi, wakati parachichi lina aina ya mafuta ambayo yana faida kwa afya.

Jedwali likionyesha kiasi cha virutubisho katika gramu 100 za
parachichi.
Aina ya kirutubisho
Kirutubisho
Kiwango kilichopo
Vitamini
Vitamini A
7ug

Vitamini E
2.1ug

Vitamini C
10mg

Thiamine
0.1mg

Niacini
1.7mg

Vitamini B 6
0.3mg

Folic acid
81ug
Madini
Kalshamu
12mg

Phosphorasi
52mg

Magnesiamu
29mg

Potasiamu
599mg

Munyu (Sodium)
7mg

Chuma
0.6mg

Zinki
0.6mg

Shaba
0.2mg

Manganizi
0.1mg
Protini muhimu
TRP(Tryptophan)
25mg

THR(Threonine)
73mg

ILE(Isoleucine)
84mg

LEU(Leucine)
143mg

LYS(Lysine)
132mg

MET(Methionine)
30mg

CYS(Cysteine)
27mg

PHE(Phenylalanine)
232mg

TYR(Tyrosine)
49mg

VAL(Valine)
107mg

ARG(Arginine)
88mg

HIS(Histidine)
49mg

Parachichi katika tafiti nyingi limeonekana kuwa na faida katika afya ya moyo. Wagonjwa wa moyo wamekuwa katika makatazo ya kutumia aina ya mafuta ambayo yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa lehemu katika damu(mafuta hayo kitaalam kama polysaturated fat), na kuongeza matumizi ya mafuta yasiyoongeza lehemu katika damu (monosaturated fat). Parachichi ni chanzo kizuri cha mafuta yasiyoongeza lehemu katika damu. Utafiti unaonyesha kuwa matumizi ya mafuta haya  katika parachi hupunguza lehemu iliyo hatari ( kitaalam kama, Low density lipoprotein), na huchangia katika ongezeko la lehemu isiyo hatari( High density lipoprotein).
Madini ya Potasiamu ni aina ambayo huwa watu hawapati ya kutosha kutoka katika vyakula. Parachichi lina kiwango kikubwa cha madini ya potassium kuliko ndizi. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa matumizi ya madini haya huambatana na kupungua kwa shinikizo la damu, shinikizo la juu la damu laweza kupelekea mtu kupata kiharusi, shambulizi la moyo hata figo kushindwa kufanya kazi.

Parachichi lina kiwango kikubwa cha fiba. Fiba ni kirutubisho kutoka katika vyakula vya jamii ya mimea, fiba huwa hazimeng’enywi tumboni lakini huwa zina umuhimu mkubwa sana, kama kusaidia kupunguza uzito wa mwili, kusaidia urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini na kupunguza hatari ya kupata magonjwa mengi mwilini. Kuna aina fulani ya fiba ambazo huwa ni virutubisho kwa ajili ya bakteria wenye faida tumboni, hii huimarisha kinga ya mwili na kusaidia mwili kufanya kazi katika kiwango kinachotakiwa. Kwa kuwa parachichi lina kiwango kikubwa cha fiba, husaidia kuboresha mmeng’enyo na kupata choo katika hali ya kawaida.

Aina ya mafuta na virutubisho tulivyoviona awali katika parachichi vinasaidia afya ya ngozi yako. Husaidia ngozi yako kutokuwa kavu na kuwa na unyevu unaotakiwa na kuifanya ngozi kuwa laini na yenye afya. Vitamini C husaidia katika kusaidia uponaji haraka wa ngozi na kujijenga upya kwa seli za ngozi zilizoharibika,husaidia kujenga elastini na collageniambazo ni muhimu katika ngozi. Uwepo wa virutubisho viondoavyo sumu(antioxidants) katika parachichi kama carotenoidi na vitamini E, hutusaidia kutukinga na mionzi mikali ya jua, kwa hiyo huzuia makunyanzi katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuwa na mwonekano mzuri wakati wote.

Tunda hili ni lishe bora kwa wale wenye kisukari. Parachichi lina kiwango kidogo cha sukari ukilinganisha na matunda mengine. Pia uwepo wa mafuta aina ya ‘monosaturated’ husaidia kuboresha ufanyaji kazi wa homoni ya insulini, katika urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini. Faida nyingine ni kuwa Vitamini C  katika parachichi husaidia kuimarisha mishipa ya damu na kuboresha kinga ya mwili ambayo ni faida kubwa kwa wagonjwa wenye kisukari.

Faida katika afya ya uzazi ni dhahiri. Parachichi lina Vitamini E ambayo ni “antioxidant”  Potasiamu, Vitamini B6,Vitamini C ambazo hutusaidia kutukinga na magonjwa ya moyo hata yale ya kisukari. Chochote kile kinachosaidia afya ya moyo pia husaidia afya ya uzazi. Wanaume wenye magonjwa ya moyo na kisukari huwa tatizo kubwa la upungufu wa nguvu za kiume.

Parachichi pia limeonekana kuwa na faida nyingi katika kuboresha afya ya macho, viungo vya mwili na nyinginezo nyingi. Katika utafiti mmoja uko Marekani, ulionyesha kuwa watu walao parachichi walionekana kuwa na afya bora ukilinganisha na wale wasiokula parachichi. Waliokula parachichi hawakupatwa  na matatizo ya mmeng’enyo  ukilinganisha na wale wasiokula. Matatizo ya mmeng’enyo huchangia watu kupatwa na magonjwa ya moyo na kisukari.


Unasubiri nini sasa? Anza kutumia matunda haya kuboresha afya yako. Unapokwenda sokoni usisahau kununua parachichi.Faida ni nyingi zitokanazo na ulaji wa tunda hili.

Tupia Comments: