Maharusi 700 waliopewa magongo
Mamia ya mabiarusi nchini India, ambao walishiriki katika harusi ya pamoja, wamepewa magongo ya mbao na kuhimizwa wayatumie kama silaha iwapo watadhalilishwa au kudhulumiwa na waume zao nyumbani.
Magongo hayo yameandikwa ujumbe, miongoni mwake "la kutumiwa dhidi ya walevi".
Magongo hayo yana ukubwa wa sentimita 40 hivi (inchi 15) na kawaida hutumiwa wakati wa kufua nguo.
Gopal Bhargava, ambaye ni waziri katika jimbo la Madhya Pradesh, amesema alitaka kuwafanya wengi wafahamu zaidi kuhusu tatizo la udhalilishaji nyumbani.
Aliwaambia wanawake kwamba wajaribu kuzungumza na waume zao na kutatua tofauti zao kwa amani kabla ya kutumia magongo hayo.
Lakini iwapo waume zao watakosa kusikiliza, wanafaa kutumia magongo hayo - ambayo India hufahamika kama mogri na hutumiwa kugonga nguo na kutoa vumbi na uchafu.
Bw Bhargava alipakia picha za mabiharusi wakiwa na magongo hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Aliambia AFP kwamba ameingiwa na wasiwasi sana kutokana na wanawake wengi maeneo ya mashambani wanaodhalilishwa na waume zao walevi.
"Wanawake husema kila waume zao wanapolewa, huwapiga. Pesa walizoweka akiba hutwaliwa na kutumiwa kwa ulevi," alisema.
"Hizi si juhudi za kuwachochea wanawake au kuwafanya wawashambulie waume zao, bali ni njia ya kuzuia dhuluma."

Bw Bhargava, ambaye ni wa chama cha Waziri Mkuu wa India Narendra Modi cha Bharatiya Janata Party, amesema ameagizia magongo karibu 10,000.
Maharusi 700 walipewa magongo hayo katika sherehe ya harusi ya pamoja mji wa Garhakota mwishoni mwa wiki.
Harusi za halaiki huandaliwa India kusaidia wanandoa wasio na pesa kufunga ndoa bila kulipia gharama kubwa ya kuandaa sherehe yao wenyewe.
Vyombo vya habari nchini humo vinasema huenda hatua hiyo ya kutoa magongo ni njia ya mwanasiasa huyo kujaribu kujipatia umaarufu kabla ya uchaguzi wa jimbo mwaka ujao.

Tupia Comments: