Saudi Arabia inataka kuacha kununua silaha kutoka Ujerumani na kujikita zaidi kwenye ushirikiano wa kiuchumi, huku Kansela Angela Merkel akiwa ziarani nchini Saudia alikokosoa ushiriki wa Saudia kwenye vita vya Yemen
Naibu Waziri wa Uchumi wa Saudia, Mohammed Al-Tawaijiri, ameliambia jarida mashuhuri la hapa Ujerumani, 'Der Spiegel', kwamba nchi yake inatambua mazingira ya kisiasa ya Ujerumani na kwa hivyo inarekebisha kipaumbele chake kwenye bidhaa inazoingiza kutoka taifa hili kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya.
Katika mahojiano yaliyochapishwa jana Jumapili katika siku ambayo Kansela Merkel alikuwa ziarani nchini Saudi Arabia, al-Tuwaijiri alisema na hapa namnukuu: "Hatutaisababishia tena serikali ya Ujerumani matatizo zaidi kwa kuomba silaha. Uhusiano na Ujerumani una umuhimu mkubwa zaidi kwetu kuliko kulumbana juu ya mikataba ya silaha." Mwisho wa kumnukuu.
Mikataba ya silaha kati ya nchi hizi mbili imekumbwa na utata kwa miaka mingi sasa, ambapo ufalme huo wa Ghuba umekuwa ukikosolewa mara kwa mara kutokana na rikodi yake ya haki za binaadamu.
Miongoni mwao ni ushiriki wake kwenye vita vya muda mrefu nchini Yemen, ambavyo vimeshuhudia raia wengi wakiuawa kwa mashambulizi ya yanayofanywa na ndege za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia. Vifo hivyo vimezuwa mjadala nchini Ujerumani kwamba silaha zake zinatumika kuuwa watu wasiokuwa na hatia.
Kwa mujibu wa takwimu za awali, mwaka 2016 pekee, Ujerumani iliiuzia Saudia silaha zenye thamani ya zaidi ya euro nusu bilioni.
Merkel ataka Saudia iwache kushambulia Yemen
Mfalme Salman wa Saudi Arabia alimpokea Kansela Angela Merkel kwa gwaride la kijeshi.
Kuchapishwa kwa mahojiano ya Al-Tuwaijiri na jarida la 'Der Spiegel' kumesadifiana na ziara ya Kansela Merkel nchini Saudia, ambaye aliwasili hapo jana na kupokelewa na kufanya mazungumzo na Mfalme Salman na maofisa wengine. Hata hivyo, kwenye ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara wa Kijerumani aliokwenda nao Kansela Merkel, hawakuwemo wawakilishi wa kampuni za silaha.
Kwenye mazungumzo ya viongozi hao mjini Jeddah, Kansela Merkel alitoa wito wa kukomeshwa kwa mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudia nchini Yemen, akisema kuwa Ujerumani inaamini kwenye mchakato unaoongozwa na Umoja wa Mataifa wa kupatikana suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo huo.
Kansela Merkel, badala yake, aliitaka Saudia kuchukuwa hatua zaidi za kuwakinga watu ambao tayari wanaishi kwenye nchi iliyoelemewa na ufukara wasiangukie kwenye hali mbaya zaidi ya kibinaadamu. 
Serikali ya Saudi Arabia imekuwa ikiingilia kwenye vita vya Yemen kwa zaidi ya miaka miwili sasa ikiongoza muungano wa mataifa ya Kisunni ya Ghuba dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaotokana na madhehebu ya Shia, ambao Saudia inasema ni mamluki wa Iran.
Hata hivyo, Iran na Houthi wenyewe wamekuwa wakikanusha kushirikiana kwenye vita hivyo vya kuwania madaraka, ambavyo hadi sasa vimeshaangamiza maisha ya maelfu ya watu na kuwageuza mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Tupia Comments: