MPIGA Picha wa Magazeti ya Serikali (TSN), Mohammed Mambo ameibuka mshindi wa tuzo ya mpigapicha bora, huku mwandishi wa gazeti hili Shadrack Sagati akiibuka mshindi wa pili katika kipengele cha uandishi wa habari za data katika Tuzo za Umahiri wa uandishi wa Habari (EJAT) mwaka 2016.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilianyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na ilihusisha vipengele 19 vilivyoshindaniwa na waandishi kutoka kwenye magazeti, radio na televisheni. Jumla ya waandishi 66 waliteuliwa kuwania tuzo hizo zinazoendeshwa na Baraza la Habari (MCT). Mambo aliibuka mshindi katika kipengele hicho cha mpigapicha bora kutokana na picha yake aliyowapiga wanafunzi wa shule ya msingi Majimatitu iliyopo wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, waliokuwa wamekaa katikati ya barabara huku nyuma yao kukiwa na maiti ya mwanafunzi mwenzao aliyegongwa na gari eneo la kivuko cha watembea kwa miguu.
Kwa upande wake, Sagati habari iliyomfanya kuwa mshindi wa pili ni iliyokuwa ikieleza kwanini gari aina ya Noah hazistahili kufanya biasahara ya kubeba abira. Washindi wa tuzo za mwaka huu waliteuliwa na majaji mbalimbali ambao ni Ndimbara Tegambwage, Hassan Mhelela, Pili Mtambalike, Dk Mzuri Issa Ali, Mwanzo Milinga, Nathan Mpangala na Dk Joyce Bazira ambaye alikuwa katibu wa jopo na Valeria Msoka ambaye alikuwa kiongozi wa jopo hilo la majaji. Kazi zilizowasilishwa MCT kwa ajili ya kushindanishwa zilikuwa zaidi ya 810, zikiwemo zaidi ya 435 kutoka vyombo vya habari vya kielektorini na kazi zaidi ya 374 kutoka kwenye magazeti.
Kazi hizo ni nyingi ikilinganisha na zile za mwaka 2015 ambako jumla ya kazi zilikuwa 568. Mshindi wa jumla wa tuzo hiyo kwa mwaka huu ni Florence Majani kutoka gazeti la Mwananchi. Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo hizo, Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Jenerali Ulimwengu ambaye pia ni mwandishi mkongwe licha ya kuwapongeza washindi aliwataka waandishi ambao hawakufanikiwa kupata tuzo kuongeza juhudi katika kazi zao. Alisema tasnia ya habari si ya watu walioshindwa masomo na kuikimbilia wakidhani ni nyepesi, bali ni taaluma inayohitaji watu mahiri na makini ambao wamejitolea kufanya mambo yasiyowahusu.
Ulimwengu aliwataka wanahabari kujituma na kuwa makini katika uandaaji wa habari na kutambua kuwa wanaofanyia kazi baadhi yao wanajua kuliko wao na pia kutotumia kigezo cha kuwa katika tasnia hiyo kudhani wanajua kuliko wao. Aidha, alitoa mwito kwa wanahabari nchini kujenga utamaduni wa kujiendeleza kielimu, lakini pia kuwa kujenga tabia ya kusoma mara kwa mara vitabu na majarida, kusikiliza na kujifunza mambo mbalimbali ili waweze kufanikiwa na kutekeleza kazi zao kwa ufanisi. Alisema mwandishi wa habari asiyependa kusoma vitabu na kujifunza kila wakati hawezi kuwa mahiri na wala kazi zake haziwezi kuwa nzuri.
Aidha, Aliwataka waandishi kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi za wanausalama na askari polisi waliowashambulia na baadae kuwadai fedha nyingi kama fidia ya matukio mabaya waliyowafanyia. Baadhi ya vipengele hivyo ni mwandishi bora wa habari za uchumi, biashara na fedha, habari za michezo na utamaduni, habari za afya, Kilimo, Elimu, habari za uchambuzi wa matukio, habari za utalii. Vingine ni mwandishi bora wa habari za Afya ya uzazi kwa vijana, habari za Ukusanyaji kodi, habari za uchunguzi, habari za takwimu, Mpiga picha bora, Mchoraji bora wa vibonzo, mpiga picha bora wa televisheni.
Tupia Comments: