MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara atapandishwa Kamati ya Maadili Aprili 21, 2017 kujibu tuhuma za utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Taarifa ya TFF kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba Manara atapewa mashtaka yake leo na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.
TFF imesema kwa mujibu wa Katiba yake, kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.
“Wanafamilia wa mpira wa miguu ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi mbalimbali,”.
“Ili kutunza heshima ya mpira wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu zote hizo ndani na nje ya uwanja,”.
“Taswira njema ya shirikisho inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho,”.
“Dhima ya uongozi wa TFF ni pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua zitachukulia,” imesema taarifa ya shirikisho hilo.
TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Manara kuishutumu TFF kufanya njama za kuihujumu Simba isitimize dhamira yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
“Sisi kama Simba, tumegundua mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya watu pale TFF, wanachotaka wao ni klabu yetu ikose ubingwa ili Yanga wauchukue na kwa taarifa yenu ni kwamba tunajua kila kitu kinachoendelea na hatutakubali kukaa kimya.
“Tunazo taarifa kwenye kile kikao cha kwanza cha Saa 72, mmoja wa viongozi wakuu wa TFF alitoa taarifa kwa mmoja wa maofisa wake akishinikiza matokeo yale yasitangazwe, ushahidi tunao, tunasubiri mamlaka halali tuuweke hadharani, ila bodi ikakataa na ikasema hiki ni kikao halali huyo ofisa yupo, tunalitaka jeshi na mamlaka nyingine kama TCRA vichunguze sakata hili,”alisema.
Alisema kama wakipokonywa pointi za mezani walizopewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kutokana na Rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu watalipeleka suala hilo ngazi za juu.
Lakini pia Manara anadaiwa kuwatolea maneno yasiyo ya kiungwana viongozi wa juu wa TFF, akiwemo Rais wake, Jamal Malinzi.
Yote haya yanatokana na Kagera Sugar kupinga uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia timu hiyo kwa madai ya kumtumia Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Utata upo katika mchezo wa Jumatano ya Januari 18, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kati ya wenyeji Kagera Sugar na African Lyon ya Dar es Salaam, ambao inadaiwa Fakhi alionyeshwa kadi ya njano wakati klabu yake inapinga.

Tupia Comments: