MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imetahadharisha wazalishaji wa bidhaa za chakula kutosambaza chakula kilichoharibika kwenda kwa wananchi na kwamba mamlaka hiyo imetangaza kuwashughulikia wasambazaji hao kama wauaji.
Akitoa mada kuhusu sheria sura ya 219 ya chakula, dawa na vipodozi ya mwaka 2016 katika kikao kazi cha waandishi wa habari, Mwanasheria Mshauri wa TFDA, Iskari Fute amesema kuwa sheria mpya za mamlaka hiyo zimezingatia namna ya kuwalinda walaji dhidi ya bidhaa zisizofaa kwa kuweka sheria kali.
Mwanasheria huyo alisema wapo baadhi ya wasambazaji wa bidhaa za vyakula kwa makusudi wakijua bidhaa wanazosambaza zimeharibika wanaamua kuuza na kupeleka bidhaa hizo kwa wananchi, jambo ambalo kisheria halikubaliki.
Awali akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo amesema katika kuunga mkono kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, jumla ya viwanda 635 vinavyozalisha bidhaa zinazosimamiwa na mamlaka hiyo vimesajiliwa, ikiwa ni miongoni mwa maombi 767 ya kuanzisha viwanda.
Mkurugenzi huyo alisema jumla ya viwanda 613 sawa na asilimia 82 ya viwanda vilivyoidhinishwa vinajihusisha na usindikaji wa bidhaa za vyakula jambo ambalo mkurugenzi huyo amesema kuwa linabainisha kuzingatiwa kwa sheria katika kusajili viwanda.
Tupia Comments: