UPELELEZI katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006 na msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu na wenzake wawili, umekamilika.
Wakili wa Serikali Maandalizi, Hellen Mushi alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa. Mushi alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji wa awali. Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi Juni mosi mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali.
Wema ambaye pia ni mfanyabiashara na wenzake wawili wanawakilishwa na Wakili Tundu Lissu. Washitakiwa wengine ni mfanyakazi wake wa ndani Angelina Msigwa (21) pamoja na mkulima Matrida Abas (16) ambao wote waliwakilishwa na Wakili Hekima Mwesigwa. Wanadaiwa walikutwa na dawa za kulevya, Februari 4, mwaka huu nyumbani kwao Kunduchi Ununio, jijini Dar es Salaam.


Ilidaiwa kuwa, siku hiyo walikutwa wakiwa na msokoto mmoja pamoja na vipisi viwili vya bangi vya gramu 1.80 ambavyo ni dawa za kulevya. Washitakiwa wote wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini kila mmoja bondi ya Sh milioni tano.

Tupia Comments: