Hotuba ya Trump katika mji wa Riyadh nchini Saudi Arabia ilikuwa na lengo la kuizika sera ya kuelekea Iran ya mtangulizi wake Barrack Obama na pia ina maana ya kuchochea mvutano katika kanda ya Mashariki ya Kati
Baina ya kile kilichotokea Tehran na Riyadh pana tafauti kubwa. Mjini Riyadh, anaonekana Donald Trump akicheza ngoma ya upanga, ngoma ya vita, huku Mfalme Salman akimpa maelekezo rais huyo wa Marekani.
Kwa upande mwingine, mjini Tehran, watu nako wanacheza ngoma hiyo mabarabarani wakishangilia ushindi mkubwa wa Rais Hassan Rouhani anayeelemea siasa za wastani dhidi ya mpinzani wake, Ebrahim Raisi, anayependelea siasa za msimamo mkali.
Furaha imetanda katika ufalme wa Saudi Arabia, ulio na utajiri wa mafuta. Hotuba ya jana ya Trump imezindua mabadiliko mapya katika sera za Marekani kuelekea dunia ya Kiarabu kwa jumla pamoja na lawama za Saudi Arabia dhidi ya rais aliyemaliza muda wake nchini Marekani, Barack Obama. Hotuba hiyo ni kama imefikisha mwisho yote hayo yaliyokuwepo.
Wakati huo huo, mkakati ya kijeshi dhidi ya wapinzani wakuu, Iran, kama ilivyokuwa wakati wa rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush kwamba eneo hilo lilichukuliwa ni la watu wabaya waliopaswa kutengwa.
Na kwa kuwa kutengwa peke yake huenda kukawa ni hatua ambayo haitoshi, Trump ameongezea mikataba ya mauzo ya silaha yenye thamani ya dola bilioni 110 katika yale aliyobeba kwenye ziara yake hiyo ya Saudi Arabia, ambayo kwa kweli ni historia katika biashara.
Ni kejeli na machungu katika nchi ambayo ni nyumbani kwa waliohusika na mauaji ya tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2001, kukuta kuwa Trump anaishutumu Iran peke yake kwamba ndiyo inayounga mkono na kusaidia vitendo vya kigaidi.
Lakini haijawahi kutajwa kwamba wenyeji wake kutoka nchi za Ghuba wamekuwa wakiwapa msaada wa fedha na silaha wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, pamoja na makundi mengine ya jihadi, kwani hata aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, alitamka wazi wazi juu ya hilo wakati alipozungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Harvard mnamo mwaka 2014.
Kwenye hotuba yake, Trump alizungumzia kuhusu amani, usalama na ustawi katika kanda hiyo. Kama kweli angalikuwa na mtazamo kama huo, mambo yangalikuwa tofauti. Kutokana na uadui wa kimkakati uliopo kati ya Iran na Saudi Arabia, hakuna tamko lolote lililoashiria kujiepusha na makabiliano au hata kuwepo na usawa.
Badala yake, rais huyo wa Marekani anachochea mapambano. Ingawa hotuba ya Trump iligusia Iran, lakini hakugusia hata kidogo juu ya mwelekeo wa uchaguzi wa Iran. Bila shaka, Hassan Rohani ni mtu wa kufuata mfumo, na ni kweli kuwa licha ya udhaifu wowote ule uliopo katika mfumo wa nchi yake, watu wana matumaini makubwa kwamba Iran itafungua zaidi haki za kiraia. Na bila shaka anahitaji msaada katika jitihada zake zakuwaondosha watu wenye misimamo mikali katika vyombo vya usalama.
Badala yake, Trump amezidi kuwatia hofu Wasaudi kwamba Iran ina ushawishi katika eneo hilo. Kimakusudi ameviunga mkono wazi vita na mauaji ya mataifa ya Ghuba katika nchi ya Yemen kama sehemu ya "vita dhidi ya ugaidi".
Kama kweli Trump angelikuwa makini kuhusu nia yake kuwa watoto, wavulana na wasichana wanastahili kukua bila hofu, wanastahili kulindwa kutokana na vurugu na chuki, basi kamwe asingeweza kuwaunga mkono wenyeji wake, Saudi Arabia. Hotuba ya Trump imebashiri ukweli mmoja tu, nao ni kuwa suala la upatanishi ni jukumu la Ulaya pekee. Lazima bara hili likatae kucheza ngoma ya upanga. Licha ya kuendelea kwa miito ya kuiwekea Iran vikwazo zaidi, pana ulazima wa kuanzisha majadiliano na kufungua njia za kiuchumi kwa Tehran.
Ulimwengu lazima ujaribu kufanya mazungumzo ya kikanda ili kuanzisha mbinu mpya za usalama ambazo zitazingatia maslahi ya pande zote husika. Usalama katika eneo la Mashariki ya Kati ni zaidi ya mchezo uliokwenda kapa. Ndio maana ilikuwa ishara nzuri pale mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, alipompongeza Hassan Rouhani kwa kuchaguliwa tena kuwa rais.
Tupia Comments: