MAMIA ya Wananchi wameudhuria mazishi ya Mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar.Vuai Ali Vuai, Marehemu Bi.Mwanaisha Hassan Vuai huko Kijijini kwao Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Mazishi hayo yameongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, aliyeambatana na viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na jamhuri ya muungano Tanzania.
Bi. Mwanaisha amefariki jana wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tasakhtaa iliyopo Vuga Mjini Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya mazishi hayo, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar, Nd. Vuai Ali Vuai alisema kifo cha Mama yake mzazi kimeacha pengo kubwa katika familia hiyo kwani marehemu huyo alikuwa akitegemewa na jamii kutokana na busara zake.
Aidha Vuai amewashukru wananchi mbali mbali waliojitokeza kumuunga mkono katika mazishi hayo na kuwasihi waendelee kuwa na umoja wa kushirikiana katika mambo mbali mbali ya kijamii.
“ Mama yetu tulimpenda sana lakini ndio hivcyo amefariki sasa kilichobaki kwetu sisi tuliobaki ni kumuombea dua yeye pamoja na wazee wetu wengine waliofariki kabla yake.”, alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Mbali na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pia Mazishi hayo yameudhuriwa na Viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Omar Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi”,Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania Shaka Hamdu Shaka, Mkuu wa Mkoa kusini Unguja Dk.Idrissa Muslim Hija, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu.
Viongozi wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrissa Kitwana Mustafa, Mnadhimu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM, Ali Salum Haji pamoja na baadhi ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Bi.Mwanaisha Hassan Vuai amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 ameacha watoto tisa (9) pamoja na wajukuu kadhaa, Mungu ailaze roho ya marehemu pahali pema peponi-Amin.
Tupia Comments: