Mlipuko huo ulitokea baada ya tamasha la muziki katika ukumbi wa Manchester Arena Jumatatu (22.05.2017) usiku. Mlipuko ulitokea wakati watu walipokuwa wakiondoka baada ya tamasha kukamilika.
Polisi nchini Uingereza wanasema watu wasiopungua 19 wameuawa na wengine 59 kujeruhiwa kwenye mlipuko uliotokea mwishoni mwa tamasha la muziki la mwanamuziki wa Marekani Ariana Grande mjini Manchester kaskazini magharibi mwa England. Maafisa wawili wa Marekani wamesema mshambuliaji wa kujitoa muhanga anashukiwa kuhusika na mlipuko huo.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema tukio hilo linachukuliwa kuwa la kigaidi. May anatarajiwa kuongoza kikao cha dharura cha kamati ya usalama kuanzia saa tatu asubuhi. Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti kwamba kulitokea milipuko miwili ndani ya ukumbi huo wenye nafasi 21,000 za watu kukaa.
Polisi wa Manchester wanasema wanashirikiana na polisi ya taifa na mashirika ya kijasusi kuchunguza mlipuko huo. Meya wa mji wa London Sadiq Khan ametuma risala zake za rambirambi kwa jamii za wahanga na amesema mji wa London unasimama pamoja na mji wa Manchester kufuatilia tukio hilo.

Tupia Comments: