Moja ya mashambulio ya kundi la Boko Haram nchini Nigeria
Mtu ambaye anafikiriwa kuwa mpiganaji wa kundi la Boko Haram amesema kundi hilo la wanamgambo wenye itikadi kali linapanga kushambulia kwa mabomu mji mkuu wa Nigeria, Abuja, katika vidio iliyopatikana na Reuters.
"Mashambulizi zaidi ya mabomu yanakuja, ikiwa ni pamoja na Abuja ambako mnahisi mko salama," amesema mtu huyo katika vidio ambayo imepatikana na waandishi habari wa Sahara, tovuti ya waandishi habari yenye makao yake nchini Marekani, na mwandishi habari wa Nigeria Ahmad Salkida.
Reuters hata hivyo hawakuweza kuthibitisha uhalali wa vidio hiyo.
Idara ya usalama wa taifa nchini Nigeria , DSS , mwezi Aprili ilisema imezuwia mipango ya wanamgambo wa Boko Haram wenye mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu kushambulia balozi za Uingereza na Marekani mjini Abuja.
Kiasi ya wasichana 82 waliachiwa huru Jumamosi iliyopita kwa kubadilishana na makamanda wa kundi la Boko Haram baada ya kushikiliwa kwa muda wa miaka mitatu. Walikuwa ni miongoni mwa kiasi wasichana 270 waliokamatwa na kundi hilo la jihadi kutoka mji wa Chibok kaskazini mashariki mwa Nigeria mwezi Aprili mwaka 2014.
Katika vidio ya pili iliyopatikana na Reuters , mmoja kati ya kundi la wanawake wanne waliojifunika nyuso zao alidai kuwa miongoni mwa wasichana waliotekwa na hataki kurejea nyumbani.
"Hatutaki kurudi kuungana na wazazi wetu kwasababu hawamuabudu Allah , na nawaomba kujiunga nasi," alisema, akishikilia bunduki na akizungumza kwa lugha ya Kihausa ambayo huzungumzwa na watu wa kaskazini mwa Nigeria. Aliongeza : "Hatukuolewa kwa kushurutishwa na mtu yeyote. "Ndoa ni utashi wa mtu."
Reuters haikuweza kuthibitisha uhalisia wa vidio hiyo.
Mpatanishi na mwanasheria Zannah Mustapha amesema baadhi ya wasichana waliotekwa walikataa kuachiliwa huru , na kuzusha hofu kwamba wamepata itikadi kali ya wapiganaji hao wa jihadi, na huenda wanajisikia woga ama aibu kurejea katika maisha yao ya zamani.
Tupia Comments: