KWA mara nyingine wabunge wamekumbushwa kuwa serikali haijazuia mikutano ya vyama vya siasa nchini, bali kilichofanyika ni kuwekewa utaratibu, jambo lililosisitizwa lipo duniani kote.
Msisitizo huo ulitolewa bungeni juzi usiku na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyesimama na kulalamikia kile alichokiita ni vyama vya siasa kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara.
Katika kujibu swali hilo, Mwigulu alisema baadhi ya Watanzania wameshindwa kumwelewa Rais John Magufuli kwa mwongozo na utaratibu alioutoa huku Waziri Mwigulu akisisitiza kuwa kamwe Rais hajazuia mikutano ya kisiasa.
Mwigulu alizidi kufafanua kuwa kilichofanyika ni mikutano ya kisiasa kuwekewa utaratibu kwa wabunge kufanya kazi na mikutano ya kisiasa katika majimbo yao. “Ni utaratibu wa kawaida kote duniani na mara nyingi inapangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi hasa yanapokuwepo majukumu na masuala ya kisiasa…majuzi vyama vyote viliruhusiwa kufanya kampeni katika uchaguzi mdogo wa wabunge na madiwani.
Nani alizuiwa?” alihoji. Akafafanua, “Kilichopo ni kwamba wachaguliwa wote mnaruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa katika majimbo yenu, ninyi ni wanasiasa, hamuwezi kuzuiwa kufanya siasa.
Nimshukuru sana Rais (Magufuli), nadhani kwa uzoefu wake kuwa bungeni na kuwa katika siasa kwa zaidi ya miaka 20, ameliona hili ndiyo maana akataka uwepo utaratibu ili watu wafanye kazi katika maeneo wanayowajibika, kule walikopigiwa kura.”
Ufafanuzi huo umekuja baada ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kudai Rais Magufuli amezuia kufanyika kwa mikutano ya kisiasa nchini hadi mwaka 2020, utakapofanyika Uchaguzi Mkuu, jambo ambalo sio kweli.
Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku mikutano ya kisiasa isiyo na tija, akiwataka wabunge kusisitiza wananchi kufanya kazi badala ya kila kukicha kuburuzwa na wanasiasa katika mikutano na maandamano.
Tupia Comments: