MBUNGE wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee (Chadema) ametangaza kubadili tabia ndani ya Bunge huku akimwangukia Spika na kuwaomba radhi Watanzania kutokana na matamshi ya kuudhi aliyoyatoa bungeni, yakiwa kinyume cha maadili na Kanuni za Bunge.
Mdee alifikia hatua hiyo juzi usiku, alipomuomba radhi kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, wabunge wa Bunge la Jamhuri na Watanzania wote kutokana na kauli yake ya kuudhi aliyoitoa ndani ya mhimili huo wa dola Aprili 4, mwaka huu, wakati mchakato wa kuwachagua wabunge wa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Katika hali iliyoonesha hisia kali na kujutia kosa lake, Mbunge huyo wa Kawe alisema amebaini kosa lake na hivyo analazimika kuwaomba msamaha Watanzania, wabunge na hususan Spika.
Alisema mbali ya kulikosea Bunge, Spika na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla, pia kuanzia sasa atakuwa makini wakati wa uchangiaji wa mada mbalimbali bungeni ili asirudie kutenda makosa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Aprili 4 mwaka huu wakati wa uchaguzi wa EALA, kuna matukio ambayo yalitokea na kunisababisha kuzungumza lugha ambayo kwa utamaduni za Bunge siyo sawa. Ilimgusa Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kigwangalla na wengine,” alisema Mdee.
Akaongeza, “Kama mbunge mzoefu, nimetumia jitihada kuzungumza na kuomba radhi wahusika katika individual capacity (nafasi ya mmoja mmoja), lakini vile vile nikaona ni busara kwa sababu haya maneno niliyasema bungeni, kuzungumza pia hapa na kumuomba radhi kwa Mheshimika Spika.
Nimeomba huu muda specifically (mahususi) kumuomba radhi, namheshimu na kumwambia sitarudia,” alisema Mbunge huyo wa Chadema. Alisema Spika ni kiongozi wake, lakini pia ni mwananchi wa Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam, hivyo kwa kuzingatia hayo mawili na kwa umakini mkubwa, anaomba radhi kwake, kwa Dk Kigwangalla, Bunge na wabunge, wananchi wa Jimbo la Kawe na kwa Watanzania kwa jumla.
“Niahidi tu kwamba michango yangu ya Bunge itaendelea kama kawaida, lakini kwa kutumia lugha za staha…,” alisema na kushangiliwa na wabunge huku wengine wakimtania kwa kupaza sauti wakisema, “Mdee sasa ameokoka.”
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alimpongeza Mdee kwa ukomavu aliouonesha na kuahidi kufikisha samahani yake kwa Spika licha ya kwamba ipo kwenye kumbukumbu za Bunge (Hansard).
Hivi karibuni, Mdee alijikuta matatani baada ya kudaiwa kutoa kauli ya kumtukana Spika Ndugai wakati wa uchaguzi huo wa EALA, na baadaye aliondoka mjini Dodoma. Spika Ndugai aliagiza popote alipo arejee na kuhojiwa na Kamati ya Kinga, Haki na Maadili ya Bunge.

Tupia Comments: