WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Serikali inatambua umuhimu wa Katiba mpya, lakini akashauri wabunge kutotumia muda na nguvu na nyingi kushinikiza mchakato wa Katiba mpya. Profesa Kabudi alisema zipo nchi zinazoheshimika duniani, lakini hazina Katiba iliyoandikwa.
Alitoa mfano wa nchi hizo kuwa ni pamoja na Uingereza na Israel, zinazoongozwa na utashi wa mila na desturi zao. Waziri huyo msomi aliyebobeba katika masuala ya sheria alisema hayo wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara yake uliowasilishwa juzi na kupitishwa baada ya mjadala mzito.
Wabunge walipitisha Bajeti iliyokuwa imeombewa na Wizara hiyo ya Sh 166,479, 908,000. Alitumia fursa hiyo kuwafunda wabunge kuhusu masuala ya kisheria na wengi wakiwemo wa kambi ya upinzani walionekana kumwelewa na hata kumshangilia mara kwa mara.
Alisema zipo nchi ambazo hazina kitabu (katiba) kilichoandikwa. Akasema, “Uingereza haina Katiba iliyoandikwa.” Waziri Kabudi akaongeza, “Ukiwauliza; mila, desturi. Israel haina Katiba iliyoandikwa. Waheshimiwa wabunge, mambo makubwa kama haya hayataki shinikizo, yanataka umuombe Mungu uwe mwerevu kama nyoka na mpole kama hua ili kufikia mahali ambapo taifa linakuwa na umoja.”
Kuhusu Kaimu Jaji Mkuu Akizungumzia suala la Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kutothibitishwa au kuondolewa baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu alipoteuliwa Januari 17, mwaka huu, aliwashauri wabunge waheshimu mamlaka ya uteuzi, kwa kuwa Rais ana mamlaka ya kumteua yeyote anayeona anafaa huku akisisitiza kuwa, hakuna ukomo wa muda wa mtu anayekaimu.
Kambi ya Upinzani Bungeni ilidai Profesa Ibrahim amekaimu nafasi hiyo kwa muda mrefu, kitu ambacho hakistahili. Profesa Kabudi akasema, “Ukiangalia Katiba, iko wazi kabisa, inamruhusu Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu na haiweki mipaka. Nalisihi Bunge liheshimu mamlaka ya uteuzi.
Rais anayo mamlaka, na Rais anavyo vigezo vingi, na Rais msidhani ni mtu anayetembea, ni taasisi, ina macho zaidi ya mawili, tuiache ifanye kazi yake, hivyo niwasihi sana wabunge, tuache Kaimu Jaji Mkuu afanye kazi yake, tusifike mahali tukamtweza. Sisi wanasheria, tuuheshimu sana mhimili huu.”
Alimshangaa Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara hiyo, Tundu Lissu kwa upotoshaji, baada ya kudai kuwa, katika historia yote tangu uhuru, Tanzania haijawahi kutokea Rais wa nchi akashindwa kuteua Jaji Mkuu kamili kujaza nafasi iliyo wazi ya Jaji Mkuu.
Alisema si kweli kwamba Tanzania haijawahi kuwa na Kaimu Jaji Mkuu, akisema baada ya Jaji wa mwisho wa Tanzania 1964/65, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, hakuona tena sababu ya kuwa na Jaji Mzungu, hivyo alianzisha jitihada za kutafuta Jaji Mwafrika na kupatikana mtu mwenye asili ya Afrika, Philip Telford Georges, raia wa Trinidad & Tobago.
Hata hivyo, alisema Georges alichelewa kuwasili nchini kuapishwa na wakati anasubiriwa, aliteuliwa Jaji Kaimu Jaji. Jaji Augustine Saidi aliyekuwa mzalendo wa kwanza kushika wadhifa huo, akifuatiwa na Francis Nyalali, Barnabas Samatta, Augustino Ramadhani, Mohamed Chande Othman aliyestaafu mapema mwaka huu na sasa nafasi hiyo inakaimiwa na Profesa Ibrahim.
“Kwa hiyo, hakuna Kaimu Jaji Mkuu anayeteuliwa bila kuapishwa kwa sababu ana mamlaka kamili ya kutimiza majukumu ya Jaji Mkuu, ndiyo maana hakuna Kaimu Jaji Mkuu ambaye haapishwi, hata Jaji Mkuu akisafiri kwa siku mbili, anayekaimu lazima aapishwe,” alifafanua.
Akaendelea, “Unajua, nafasi ya rais inagombewa, anachaguliwa. Tanzania tunapiga kura kumpata Rais, Rais wa Afrika Kusini hapigiwi kura anachaguliwa na wabunge kama alivyo kwa Waziri Mkuu, ndiyo maana kule Afrika Kusini chama tawala kina nguvu zaidi, ndicho kilichomwondoa Mbeki (Thabo), hakupigiwa kura na wanachi, lakini Rais wa Tanzania anapigiwa kura.
Hata Zuma (Jacob) muda wowote chama kinaweza kuamua aondoke.” “Spika wa Bunge anapigiwa kura, mtu pekee wa mhimili asiyepigiwa kura, anateuliwa ni Jaji Mkuu. Mnajua kwanini, ni msingi wa kuhakikisha mtu huyu anayeteuliwa kushika nafasi hiyo aache anakuwa na uhuru kamili,” alisema na kuwataka wabunge kuiheshimu nafasi hiyo.
Kuhusu Rais Alisema Watanzania wengine hawaielewi nafasi ya Rais. Alipambanua kuwa Rais ana nafasi tatu, ya Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na tatu ni Amiri Jeshi Mkuu. Alisema Rais ni taswira ya nchi, hivyo ana madaraka yanayompa hadhi tofauti ambayo haistahili kubezwa na ndiyo maana Bunge kwa Kanuni limezuia.
“Rais kwa nafasi yake ni taswira ya nchi; Malkia Uingereza kwa nafasi yake ya mkuu wa nchi yeye ni taswira ya nchi… na kwa maana hiyo, yeye ndiye alama ya umoja, yeye ndiye uhuru wa nchi na mamlaka yake… na kumwonesha yeye ni alama ya umoja wa nchi, ndiyo maana Rais ni peke yake anayefuatana na mtu anaitwa mpambe, anayevaa mavazi ya kijeshi… anawaonesha huyu ndiye alama ya serikali.”
“Kwa sababu hiyo, Rais ana dhamana ya kukuza na kuhifadhi umoja wa kitaifa. Sasa, ukiangalia madaraka ya Mkuu wa Nchi, yale huwezi kuyapunguza, lakini ukiangalia mamlaka yake ya Amri Jeshi Mkuu, huwezi kuyapunguza, na pia ukiangalia mamlaka yake kama Mkuu wa Serikali, kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, majukumu ya Rais akiwa Mkuu wa serikali, hayo unaweza kuyapunguza, unaweza kuyasimamia,” alieleza.
Tupia Comments: