RAIS John Magufuli (pichani) ameapa kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa nguvu zake zote, huku akiapa yeyote akayejaribu kuleta chokochoko za kutaka kuuvunja, atavunjika yeye kabla ya Muungano.
Akizungumza katika hotuba fupi ya dakika 17 jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa ambako sherehe za Muungano zimefanyika kwa mara ya kwanza tangu Uhuru na pia kwa mara ya kwanza tangu Serikali ihamishie rasmi makao makuu ya nchi Dodoma kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, alisema kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, watafanya kila linalowezekana kuhakikisha Muungano unazidi kuimarika, badala ya kuvunjikia mikononi mwao.
“Nataka niwahakikishie, mimi na Dk Shein tutaulinda kwa nguvu zote Muungano huu, na kamwe asijitokeze mtu yeyote, atakayekaidi au kujaribu kuvunja Muungano, atavunjika yeye…,” alisema Dk Magufuli.
Alisema kufikisha umri wa miaka 53 ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania si jambo dogo, kwani mataifa mengi yamejaribu kufanya hivyo, lakini bila ya kufanikiwa, huku akisisitiza kwa kusema,”Hii ni siku ya kipekee, ya kihistoria kwa tanzania.
Leo ni Bethidei (siku ya kuzaliwa) ya Tanzania.”
Aliongeza kuwa, si jambo dogo kusherehekea Miaka 53 ya Muungano, kwani kazi ya kuulinda Muungano ni ngumu, kwa sababu hata kulinda ndoa ni ngumu. “Hii inathibitisha kuwa suala la kulinda Muungano si jambo rahisi hata kidogo, hivyo basi hatuna budi kuwapongeza waliofanikisha nchi yetu kufikisha miaka 53, tunawapongeza sana.
“Tunafahamu wapo wengi waliotoa mchango wao, lakini kwa leo nitawataja wote. Wa kwanza kwa niaba yenu, napenda niwashukuru waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume kwa kuufanikisha na kuuwezesha Muungano huu.
Hawa ndio waliosaini hati ya Muungano, bahati nzuri, leo hii tunao hapa Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume,” alieleza. Aliwapongeza pia viongozi wote wa nchi katika awamu zote, Ali Hassan Mwinyi aliyeiongoza Serikali ya Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu na Jakaya Kikwete aliyeiongoza Awamu ya Nne, lakini pia waasisi mbalimbali.
Alirudia kuahidi yeye na Dk Shein, watafuata nyayo za kuulinda na kuutetea Muungano huo. Aidha, alisema wakati Watanzania wakisherehekea kutimiza miaka 53 ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania, ni vyema watu kutafakari walikotoka, walipo na wanakokwenda.
“Niwaombe pia baada ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania mwaka 1964 na leo tunatimiza miaka 53, ni ushahidi Watanzania wengi tunaoishi, ambao ni asilimia kubwa wamezaliwa baada ya Muungano, kwa hiyo tuna wajibu mkubwa, bila kujali makabila yetu, vyama vyetu na maeneo yetu, kuulinda na kuudumisha Muungano huu ili taifa la Tanzania liendelee kudumu,” alisema.
Alisema anafahamu kukiwa na mshikamano, itawezekana kuulinda Muungano, hivyo kushauri Watanzania wazidi kushikamana ili kuwe na miaka mingine mingi zaidi ya kusherehekea Muungano.
Changamoto za Muungano
Alisema licha ya mafanikio, bado zipo changamoto za Muungano, lakini akaahidi kuwa zinashughulikiwa kwa kuwa kuna Kamati ya Pamoja inayoshughulikia masuala ya Muungano ambayo Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu na wajumbe ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, mawaziri na makatibu wakuu wa Serikali zote mbili.
Alisema kamati hiyo inafanya kazi nzuri, lakini pia haipaswi kuachwa ifanye kazi peke yake, hivyo kila Mtanzania awe mshiriki wa kulinda Muungano. Alisema dhamira hiyo inashabihiana na kaulimbiu ya sherehe za mwaka huu, inayosema “Miaka 53 ya Muungano; “Tuulinde, Kuuimarisha.Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii.”
Kuhamia Dodoma
Alisema kufanyika kwa sherehe hizo mkoani Dodoma kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) imedhamiria kwa dhati kuhakikisha makao makuu ya serikali yanahamia Dodoma.
“Na niwahakikishie wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla, serikali sasa imefika Dodoma na hatutarudi nyuma tena. Kama tulivyoahidi kufikia mwaka 2020 serikali yote itakuwa imehamia hapa,” alisema Dk Magufuli na kushangiliwa mno.
Rais Magufuli ambaye mwaka jana alifuta sherehe za miaka 52 ya Muungano na kupeleka fedha kiasi cha Sh bilioni mbili katika shughuli ya upanuzi wa barabara ya Uwanja wa Ndege jijini Mwanza, alisema katika kuthibitisha utayari wa kuhamia Dodoma, tayari hatua kadhaa zimefanyika.
Alizitaja kuwa ni pamoja na mawaziri wote, manaibu waziri, makatibu wakuu, manaibu na wakurugenzi mbalimbali wameshahamia Dodoma. Alisema zaidi ya watumishi wa umma 3,000 wameshahamia Dodoma.
Lakini pia alisema awamu ya pili na ya tatu ya kuhamia Diodoma imepangwa kuhamia katika mwaka ujao wa fedha, ambapo serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh bilioni 200 kwa ujenzi wa ofisi na nyumba za viongozi wa Serikali.
Aidha, amesema juhudi za kujenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo ya upanuzi uwanja wa ndege, lakini pia ujenzi wa reli ya kisasa itakapita Dodoma, ujenzi wa barabara unaendelea sehemu mbalimbali, upatikanaji umeme, huduma za afya, elimu lakini pia maandalizi ya ujenzi wa uwanja mkubwa na wa kisasa wa michezo utakaojengwa na Serikali ya Morocco.
“Yote haya yanalenga kukidhi mahitaji ya kuwa makao makuu ya nchi,” alisema na kuwataka wakazi wa Dodoma na mikoa jirani Singida, Arusha, Manyara, Iringa na Morogoro, kujipanga kutumia fursa za Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
Pamoja na dhamira nzuri ya serikali ya kutaka kuulinda Muungano, alisema hiyo itakuwa kazi bure kama nchi haitakuwa na amani na kusema kama waasisi wasingeweza kulinda amani, leo hii Watanzania wasingekuwa na chereko za miaka 53 ya Muungano, hivyo kusisitiza kila mmoja ashiriki kuilinda amaniya nchi iliyopo.
Faida za Muungano
Alisema licha ya awali kuwapo kwa mwingiliano baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar, miaka 53 ya Muungano, nchi imekuwa na faida nyingi zaidi, mojawapo ikiwa kuwa taifa lenye nguvu, hivyo kuwezesha kulinda uhuru, amani na umoja.
Alisema nchi imekuwa yenye amani na mipaka iko salama. Aidha, alisema Muungano umewezesha mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. “Serikali zetu mbili zimefanya jitihada za kiuchumi na pia kukabiliana na matatizo ya kimasikini na ukosefu wa ajira.
Mambo mbalimbali yameimarika, demokrasia pia imeimarika. Tanzania ya sasa si ile ya mwaka 1964. Lakini pia tunaheshimika kimataifa. “Jamani, tusione vyaelea, vimeundwa na kuna watu wamefanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Muungano huu unadumu,” alisema na kuongeza kuwa, nchi imekuwa yenye heshima kubwa kimataifa imekuwa ikisaidia katika shughuli za ukombozi na kutafuta amani katika nchi mbalimbali kikanda na duniani kwa ujumla.

Tupia Comments: