Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji kwa mahojiano baada ya kukutwa na jora 43 za sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na mihuri 39 ya kampuni tofauti tofauti.
Akithibitisha taarifa hizo Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Kamanda Lucas Mkondya amesema Manji anashikiliwa na jeshi hilo tangu Julai mosi baada ya kukutwa na vitu hivyo katika ghala lake la Quality Motors, lililopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
“Ni kweli tunamshikilia tangu Jumamosi tunaendelea kumhoji kwa vitu alivyokutwa navyo ili atuambie alivipataje na anavyo kwa madhumuni gani wakati yeye sio mwanajeshi na amekaa navyo kwake,” amesema Kamanda Mkondya.
Akizungumzia endapo Manji atafikishwa mahakamani baada ya mahojiano, Kaimu Kamanda Mkondya amesema baada ya kukamilisha mahojiano na kupata taarifa kamili, wataangalia kama atapelekwa mahakamani kutokana na majibu yake.
“Tunasubiri tumalize mahojiano tupate na maelezo yake ili tuone yamekwendaje na kama atafikishwa mahakamani kulingana na mahojiano yatakavyokwenda,” amesema Kamanda Mkondya.
Hii sio mara ya kwanza kwa Manji kushikiliwa na Jeshi la polisi kwa mahojiano kwani mwezi Februari mwaka huu, alishikiliwa kwa mahojiano baada ya kudaiwa kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya.
Tupia Comments: