UTANGULIZI:                       
1. Mheshimiwa Spika, leo tumefika mwisho wa Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ulioanza Jumanne ya tarehe 4 Aprili, 2017. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii, tena baada ya kuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba kikamilifu na kwa umahiri mkubwa.

Huu ulikuwa ni Mkutano muhimu sana kwa nchi yetu kutokana na jukumu kubwa la kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 ulioanza tangu tarehe 1 Julai, 2017. Bajeti hii ambayo ni nzuri na ya kihistoria ni ya pili tu kati ya takribani Bajeti tano za Serikali ya Awamu ya Tano zitakazoandaliwa hadi kifikia Mwaka wa Fedha 2020/2021.

2.           Mheshimiwa Spika, wakati Bunge lako likiendelea, tarehe 13 Aprili, 2017 tulipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya askari polisi wetu 8 waliopoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa kwa kuuawa na kundi la wahalifu katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilayani Kibiti mkoani Pwani. Askari hao waliopoteza maisha ni Inspekta Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub. Pia, hivi karibuni mwezi Juni, 2017 Askari wetu wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani walivamiwa na kupigwa risasi na majambazi katika Kijiji cha Bungu “B” kilichopo Wilayani Kibiti. Aidha, wananchi wetu wengi wamepoteza maisha kutokana na uhalifu unaofanywa na majambazi waliopo katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

3.           Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kulaani kitendo hicho cha kihalifu, na kutoa pole kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kuondokewa na vijana hao shupavu. Aidha, natoa pole kwa familia za wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa wao. Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu hayakubaliki na wala hayavumiliki, kwani Askari ndio walinzi wetu sisi pamoja na mali zetu. Aidha, tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio kwetu sote, hivyo, Serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza kukimbia, lakini hawataweza kujificha daima. Tutawakamata!.

4.           Mheshimiwa Spika, asubuhi ya tarehe 6 Mei, 2017, nchi yetu iliamka na simanzi kubwa kufuatia ajali iliyogharimu maisha ya watu 36, wakiwemo wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wao, waliokuwa kwenye safari ya kimasomo Wilayani Karatu. Ajali hiyo imezima ndoto za vijana hao na kuacha vilio kwenye familia zao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema Peponi roho za marehemu. Aidha, nawaomba wazazi, walezi, walimu na marafiki wa watoto hao waendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwa mtihani huo mkubwa walioupata. Naendelea kutoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika na ukaguzi wa vyombo vya moto vya usafiri kwa wanafunzi na abiria wafanye ukaguzi wa kina na wa mara kwa mara ili kuliepusha Taifa na ajali zinazoweza kuzuilika.

5.           Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia ilipata pigo la kuondokewa na watumishi wawili wastaafu waliolitumikia Taifa hili kwa umahiri na uadilifu mkubwa. Watumishi hao ni marehemu Paul Sozigwa, aliyekuwa Katibu wa Rais wa Awamu ya Kwanza; na Marehemu Said Mwambungu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. Namwomba Mwenyezi Mungu awape pumziko la amani marehemu wote baada ya kulitumikia Taifa letu kwa utumishi uliotukuka na umahiri mkubwa.

SHUGHULI ZA BUNGE

6.           Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limejadili na kupitisha bajeti za Wizara zote 19 na Bajeti nzima ya Serikali Kuu, kupitisha Maazimio matano (5) ya kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kupitisha Miswada ya Sheria mbalimbali, ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi; Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka, 2017; Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017; Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi, 2017; na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili.

7.           Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 499 ya msingi na mengine 1,834 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Vilevile, katika kipindi hiki Ofisi ya Bunge iliendesha Semina mbalimbali kwa Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa uelewa mpana wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.

8.           Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu pia lilipata fursa ya kuchagua Wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo Wabunge tisa walichaguliwa. Kati ya Wabunge hao, watano ni wanawake, na wanne ni wanaume. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge hao wataiwakilisha vema nchi yetu na kwamba watatimiza kikamilifu wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaelekezwa kufanya kazi kwa karibu na Wabunge hao ikiwa ni pamoja na kuwapa ushirikiano unaostahili ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao kwenye Bunge hilo.

9.           Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na Watendaji na Wataalam wa Serikali pamoja na watumishi wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa kwenye Mkutano huu tena kwa ufanisi mkubwa.

10.        Ninawapongeza pia na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa maelezo mazuri ya ufafanuzi waliyotoa wakati wa kujibu maswali mengi ya msingi na ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu hoja za Kamati za Kudumu za Bunge na hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge binafsi ndani ya Bunge zima. Serikali inathamini sana maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, na tunaahidi kuendelea kuzingatia maoni na ushauri wao.

Tupia Comments: