UONGOZI wa Chuo cha urubani cha Shenyang (SAU) kilichopo China, kimekubali kuchangia asilimia 57 ya gharama za kusafirisha maiti endapo mwanafunzi wa kitanzania atafariki dunia akiwa masomoni nchini humo.
Hatua hiyo imetokana na malalamiko ya muda mrefu ya wazazi ambao watoto wao wanaosoma katika chuo hicho, waliolalamikia gharama kubwa ya matibabu na kusafirisha miili ya wanafunzi anapoteteza mmoja wao ameaga dunia akiwa masomoni.
Kutokana na malalamiko ya wazazi, kampuni inayojishughulisha na huduma za udahili wanafunzi wenye uhitaji wa kusoma nje ya nchi (GEL) waliuita uongozi wa chuo ili kufanya mazungumzo na wazazi.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa chuo hicho, Shi Guangda alisema chuo chake kitachangia asilimia 57 ya gharama za kusafirisha mwili wa mwanafunzi anayeaga dunia.
Awali, wazazi walilalamikia gharama kubwa za kusafirisha maiti zinazofikia Sh milioni 47 unapotokea msiba jambo ambalo ni mzigo mkubwa kwa familia.
Aidha, Guangda aliwataka wazazi kulipa dola za Marekani 100 zitakazotumika kubeba gharama za matibabu kwa wanafunzi na kusisitiza kuwa bima hiyo itatumika pale mwanafunzi atakapolazwa katika hospitali kubwa ambazo zinatambulika na chuo na si vinginevyo.
Awali, mzazi Flaurence Siyame alilalamika juu ya hatua ya wanafunzi kutibiwa kwa vigezo vya wanafunzi wa kimataifa na kuwekewa masharti mengi huku wazazi wakiwa wanalipa ada kubwa.
Aliutaka uongozi wa chuo kuweka wazi hospitali ambazo wanafunzi wanapaswa kutibiwa na kuwapa kadi itakayomfanya mwanafunzi apate matibabu kwa urahisi wakati wowote na akiwa eneo lolote.
Naye Mkurugenzi wa GEL, Abdulmalik Mollel waliwataka wazazi kuwa na utaratibu wa kufuatilia mienendo ya watoto wao wawapo vyuoni, kwani baadhi wamekuwa wakitumia mwanya wa kuwa mbali na nyumbani kufanya mambo yasiyofaa na kuongeza kuwa lengo la GEL in kutoa wanafunzi walio bora, wanaoweza kukubalika katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Aidha, aliwataka wazazi wapatapo taarifa za watoto wao kupata matatizo wawasiliane na kampuni yake au uongozi wa chuo, kwani baadhi wamekuwa wakiwadanganya wazazi ili kujipatia fedha za kufanyia starehe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege ya Air Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi aliwapa wazazi hao nafasi ya kuwapeleka watoto wao kufanya mafunzo kwa vitendo.

Tupia Comments: