Serikali ya Zanzibar imesema ni matarajio yake kuwa ifikapo Juni 2018, deni lote la Sh65.6 bilioni wanalodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), litakuwa limekamilika kulipwa.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed alisema hayo juzi katika kikao cha Baraza la Wawakilishi alipowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema katika hatua za awali, Serikali italipatia Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) Sh1 bilioni kila mwezi ili nao waongeze Sh2 bilioni na kuzipeleka Tanesco hivyo kufanya malipo kwa mwezi kuwa Sh3 bilioni.
Juhudi hizo alisema zinaweza kufanikiwa kwa mujibu wa utaratibu waliojiwekea wa kulipa deni hilo ambalo ni lazima lilipwe.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2017/18 wanatarajia pia kutumia Sh57.2 bilioni katika uanzishaji wa miradi ya jamii na ya kitaifa.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh1.58 bilioni zitatumika kuvuta umeme katika kisiwa cha Kokota baada ya kukamilika kwa kazi kama hiyo katika kisiwa cha Fundo kilichopo Pemba.
Katika hatua nyingine, Dk Khalid alisema Serikali imedhamiria kufuta ada ya biashara katika uingizaji wa malighafi na pembejeo za viwandani ili kuvutia uwekezaji na kuongeza uwezo wa ushindani.
Alisema hatua hiyo inatarajiwa kuendeleza sekta ya viwanda na kuwavutia wawekezaji walio nje.
Waziri alisema Serikali inapendekeza kutoza kodi kwenye ada au kamisheni inayotozwa na benki katika huduma zake za fedha.
Dk Khalid alisema hilo linatokana na kubaini benki zimekuwa zikitoza kodi kwa huduma za benki zinazotolewa Zanzibar bila Serikali kufaidika. Alisema ili kuzuia ukwepaji huo wa kodi kwenye mishahara unaotokana na malipo ya fedha taslim, malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa kudumu wakiwamo wa sekta binafsi, italipiwa benki. Alisema Serikali inatarajia kukusanya Sh600 milioni kutokana na kodi hiyo.
Tupia Comments: