MUFTI wa Tanzania na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeiry Bin Ally amehimiza umoja, upendo na mshikamano kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla; na pia amewataka kulinda amani ya nchi.
Pia, amesema Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) lina mipango mikubwa ya kuinua miradi mbalimbali ya maendeleo. Hali kadhalika, Mufti ameomba viongozi wa dini nchini, kufanya dua ndogo na kubwa katika kuliombea taifa na Rais Dk John Magufuli kwa moyo wa uzalendo katika kuleta maendeleo bila kujali itikadi za dini, siasa na ukabila. Alisema hayo kwenye Baraza la Idd, lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Idd.
Kuhusu maboresho ya uongozi wa Bakwata, Mufti alisema baraza limekuwa imara zaidi kwa kushirikisha taasisi zote za Kiislamu, jambo ambalo linaepusha misuguano isiyo na tija mara kwa mara. Alisema baraza lina wasomi wa kada zote na kutaka Waislamu wenye mawazo na nia ya kujenga maendeleo ya Waislamu na taifa kwa ujumla, kujitokeza na ushauri wao utazingatiwa na kupewa nafasi stahili.
Nayo risala ya Bakwata ilieleza kuwa Tume ya Kufuatilia Mali za Waislamu, iliyoundwa na Mufti mwezi Agosti mwaka jana ilitembelea mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Kilimanjaro. Kwamba tayari Tume hiyo imekabidhi ripoti yake ya kwanza na ya pili kwa Mufti. Taarifa hiyo ilisema baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Tume hiyo ya Mufti itaendelea na kazi zake katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Kigoma. Ilitaka mabaraza ya misikiti kuheshimu katiba zao na kutumia hekima na busara katika kutatua matatizo mbalimbali.
Pia, ikisema kuwa mwaka huu, Bakwata itapeleka Waislamu kwenye hija katika miji mitakatifu ya Mecca na Madina kwa bei nafuu ya dola 3,900 kwa ajili ya gharama za hija. Taarifa hiyo ya Bakwata ilitaka Waislamu wote nchini, kusaidia kujenga umoja na uhusiano kati ya Waislamu na Waislamu, na Waislamu na watu wasiokuwa Waislamu. Akitoa tafsiri ya Kurani Tukufu kwenye Baraza la Idd, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shehe Shaaban Juma alisema kila nguzo katika Uislamu, inapaswa kufuatwa na kwamba mtu akiharibu nguzo moja tu, anakuwa ameharibu nguzo zote tano.
Alisema siku ya kiama, watatokea watu wenye thawabu kama milima ya Usambara ama Upareni na akawataka Waislamu wote nchini, wadumu katika kutenda mema ili wapate thawabu. Mapema, akitoa khutba katika swala ya Idd iliyoswaliwa kwenye msikiti huohuo wa Masjid Riadha, Shehe Mlewa Shaban alisema sikukuu ya Idd ni siku ya kujiepusha na dhambi kama ulevi, kamari na lugha chafu, bali aliwataka waumini wote waitumie siku hiyo kuwapa furaha masikini, yatima na wajane. “Mtu asiseme mwezi wa Ramadhan umepita, sasa narudia mambo yangu ya zamani.
Adhabu za Mwenyezi Mungu hazina mipaka na wale waliotulizana watapata thawabu yao, kumbukeni neema na Mwenyezi Mungu na mcheni Mwenyezi Mungu. “Kitu tunachopaswa kufanya kila wakati ni kumcha Mwenyezi Mungu. Lazima tupendane, tuondoe tofauti zetu na tuujenge Uislamu. Hatuwezi kuujenga Uislamu kama hatupendani. Lazima tuilinde ibada yetu kwa sababu hatuna garantii, ni lini tutaondoka,” alisema.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof Jumanne Maghembe, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, IGP mstaafu, Said Mwema, Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael, wakuu wa wilaya za mkoa hwa Kilimanjaro na viongozi mbalimbali wa dini na serikali.

Tupia Comments: