BALOZI wa China nchini, Dk Lu Youqing amempongeza Rais John Magufuli na Serikali yake, kwa bajeti nzuri iliyowasilishwa juzi bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
Alitoa pongezi hizo Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, ambapo alisema bajeti iliyowasilishwa imeakisi dhamira ya kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ujenzi wa viwanda.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuwasilishwa kwa bajeti nzuri, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara na hivyo kuwavutia wadau wengi wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF), ambao wamekuwa wakishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na yenye umuhimu mkubwa.
Dk Youqing alibainisha kuwa Tanzania ni mahali pa kipaumbele kwa uwekezaji kutoka China na kwamba Serikali ya China itaendelea kuwashawishi wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kuzalishaji ajira nyingi zaidi kwa Watanzania.
Amesema katika bajeti ijayo, China itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kusaidia miradi inayohitajika kwa haraka katika maendeleo ya nchi, yenye matokeo mazuri katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuongeza ukusanyaji wa kodi.
Rais amefufua matumaini Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Rais John Magufuli ndani ya kipindi kifupi cha miezi 18 ya uongozi wake, amefanya mambo makubwa na mengi yamefufua matumaini na ari ya wananchi wengi, lakini kwa wachache yamekuwa machungu.
Amesema Rais Magufuli ni kiongozi ambaye amejielekeza kuijenga Tanzania mpya, ana moyo thabiti, nia njema na kujifunga kuwatumikia Watanzania wote na hasa wanyonge; na ana dhamira ya dhati ya kusimamia utendaji uliotukuka.
Akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 bungeni mjini Dodoma juzi, Dk Mpango alisema sasa Watanzania wameanza kuona matokeo ya kazi nzuri, inayofanywa na Rais Magufuli aliyeingia madarani Oktoba 2015.
Aliyarejea mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Magufuli ni pamoja na kutengua uteuzi wa viongozi mbalimbali, ambao aliona hawaendi na dhamira na kasi yake; kukamata makontena yaliyoondolewa bandarini bila kulipa kodi stahiki; kuondoa serikalini watumishi wasio na sifa/vyeti halali na wanafunzi hewa.
Mengi ni kuimarisha matumizi ya fedha za umma; kudhibiti mishahara na madai hewa; kurejesha nidhamu kwa wizara, idara na taasisi za serikali kulipa madeni ya umeme, maji na huduma nyingine; kugharamia elimu msingi bila malipo; kuongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa Sh bilioni 800 kwa mwezi hadi wastani wa Sh trilioni 1.2; kuthubutu kutekeleza uamuzi wa muda mrefu wa kuhamishia makao makuu ya serikali Dodoma.
“Kumtaka kila Mtanzania afanye kazi; kuanza utekelezaji wa kujenga Standard Gauge Railway (SGR); kununua ndege mbili mpya na kufanya malipo ya awali kwa ndege nyingine nne ili kufufua shirika la ndege na kuinua utalii; kushawishi Serikali ya Uganda kuridhia mradi mkubwa wa bomba la mafuta lijengwe kutoka Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga katika mazingira ya ushindani mkali,” alisema Dk Mpango na kushangiliwa kwa nguvu na kwa muda mrefu na wabunge.
Alisema Rais Magufuli ameendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali nchini, ikiwemo flyover Tazara, Interchange Ubungo; na ujenzi wa miradi ya miundombinu ya umeme, maji, na meli mpya mbili katika Ziwa Nyasa.
Aidha, alisema katika uongozi wake, ajenda ya kujenga uchumi wa viwanda imepata mwitikio mkubwa wa sekta binafsi nchini na hususan ukanda wa Pwani. “Ninafurahi kuwaambia Watanzania wenzangu kuwa hatua hizo ni uwekezaji wa lazima na wa busara (sensible investment).
Bajeti hii ya 2017/18 itaendelea kuimarisha matokeo haya na kuchukua hatua zaidi ili tuende mbele. Ukiona vinaelea, ujue vimeundwa! “Rai yangu kwa Watanzania wenzangu, na hasa sisi viongozi na wananchi wote ni lazima tujitoe kuijenga Tanzania, tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa tukijielekeza kutekeleza Dira na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga ustawi wa uchumi imara unaotengeneza ajira, fursa mpya na mgawanyo wa haki na usawa wa rasilimali za Tanzania kwa wananchi wote,” alieleza Dk Mpango ambaye aliwasilisha kwa umahiri hotuba ya Bajeti.
Aliwataka Watanzania walinde umoja na amani kama mboni ya jicho na tena, “letu liwe moja katika masuala yote yenye maslahi kwa taifa letu.” “Naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya serikali kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa wananchi wote ambao wanalipa kodi stahiki ambao ndiyo wamefanikisha maendeleo hayo niliyoyataja.
Serikali inawaahidi kutumia vizuri mapato yatokanayo na kodi zenu kuwaletea maendeleo. Wale mnaojaribu kukwepa kodi, mkono wa sheria utachukua mkondo wake,” alieleza Dk Mpango. Aidha, alisema ili kufanikiwa kwa bajeti hiyo ya Sh trilioni 31.71, kunahitaji nidhamu ya hali ya juu katika usimamizi wa mapato na matumizi.
Wachumi, wasomi waifagilia Wasomi, wachumi, viongozi wa dini na wafanyabiashara, wameendelea kupongeza bajeti hiyo wakisema ni nzuri, yenye mwelekeo wa kumwinua Mtanzania na kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Askofu wa Kanisa la Methodist Jimbo la Dodoma, Joseph Bundala akaenda mbali zaidi na kusema ni ya aina yake tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, wakati Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustino Mrema akisifu na kusema anaamini sasa magereza nchini zitapumua, kwani hazitapokea wahalifu wengi kutokana na bajeti kutoa fursa za watu kujiajiri.
Waliyasema hayo kwa nyakati tofauti jana, walipokuwa wanaichambua bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, iliyowasilishwa bungeni juzi na kupokelewa kwa kishindo karibu na wabunge wote.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, Makamu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini Dar es Salaam, Dk Wetengere Kitojo, mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani kwa Watu Wenye Ulemavu nchini, Jutoram Kabatele, nao wamesifu, wakisemabajeti imemeba utu wa watu na kulenga ulinzi wa soko la ndani kama itatekelezwa.
Profesa Ngowi alisema anaipongeza bajeti ya mwaka huu kwa kuwa inaonesha mwelekeo na nia thabiti ya kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda, hivyo inahitaji nguvu na utashi katika utekelezaji wake.
“Nimefurahishwa sana kwa kuwa hatua nyingi zinaonesha nia thabiti ya kulinda soko la mazao na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi ndiyo maana nyingi zimeondolewa kodi ili zipunguzwe bei na kuvutia wateja, huku za nje zikipandishiwa kodi hiyo.
Hili ni jambo la kupongeza ili bidhaa zinazozalishwa ndani zitumike zaidi kuliko zinazoagizwa nje,” alisema. “Hii pia itasaidia kulinda viwanda, lakini changamoto na shaka kubwa iliyopo ni utekelezaji wa bajeti hii kutoka mipango ya kwenye karatasi, na kuitafsiri katika utekelezaji halisi,” alisema Profesa Ngowi.
Msomi huyo mbobezi katika uchumi alisema ongezeko la kodi katika bidhaa mbalimbali zisizo za lazima katika maisha ya watu kama sigara na pombe, ni lazima ili nchi ipate mapato yake ya ndani.
Kadhalika, msomi huyo alishauri ujenzi na uimarishaji wa miundombinu uwekwe zaidi katika ubia na sekta binafsi (PPP) kama inavyofanyika katika baadhi ya madaraja na miundombinu mingine ndani na nje ya nchi.
“Ningeshauri badala ya kodi ya ardhi na majengo kukusanywa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), ingeachwa kwa serikali za mitaa maana ndio wanaojua umiliki na matumizi halisi ya majengo na ardhi kuliko TRA ambao lazima waoneshwe na zitumike gharama,” alisema.
Naye Dk Kitojo ambaye pia ni mchumi kitaaluma, alisema bajeti ya mwaka huu inaonesha Tanzania imenuia kwa dhati kuingia katika uchumi wa viwanda. Alisema maeneo yaliyopewa kipaumbele, yanaunga mkono na kuelekezwa katika ujenzi wa reli ya kati, ujenzi wa miundombinu ya makaa ya mawe na gesi na kuvutia wawekezaji mambo ambayo ni muhimu katika nchi inayojikita katika uchumi wa viwanda.
“Kodi nazo zinaonekana zimekusudiwa kuboresha uchumi wa viwanda kwa kuvuitia uwekezaji ili waingie kwa urahisi huku wakifuata taratibu na mizigo yao isafirishwe bila shida,” alisema Kitojo.
Kuhusu kuondolewa kwa baadhi ya kodi alisema, “Serikali imeondoa kodi ya leseni za barabara kwa magari; imefanya vizuri maana zilikuwa zinaumizia watu, na sasa, faida ya uamuzi huo na kuuhamishia katika mafuta ni kwamba, unalipa kodi kadiri unavyotumia; mtumiaji mkubwa wa mafuta kupitia gari lake, analipia zaidi kuliko anayetumia kidogo.”
“Hii ni jambo jema maana kabla ya hapo watu walikuwa wanalazimika kulipia magari hata kama hayatumiki na yanazidi kuharibika.” Hata hivyo alisema kuongezwa kwa kodi katika mafuta kuna hatari ya kuchochea mlipuko wa mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma mbalimbali.
“Kitu kikubwa nikionacho ni kwamba sijaona mkakati imara wa kusimamia makusanyo na kuhakikisha mapato hayo yanakusanywa kama yalivyokusudiwa ili bajeti itekelezeke sawia,” alisema.
Naye mfanyabiashara Azim Dewji alisema bajeti hiyo imedhihirisha kuwa yaliyokuwa yanasemwa na baadhi ya watu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, haina nia njema na wawekezaji, ni uzushi mtupu unaopaswa kupuuzwa na wote.
“Kulikuwa na hisia hasi kuwa Serikali haina ni nzuri kwa wawekezaji, hii sio kweli na tunaishukuru sana Serikali maana kila mtu ameona ukweli… lazima sote tujue kuwa hakuna nchi duniani inayojiendesha bila kodi, la msingi kodi ilipwe kwa haki sio kubambikwa,” alisema Dewji.
Akizungumzia kodi ya kila mwaka ya leseni ya magari iliyohamishiwa katika ununuzi wa mafuta, Dewji alisema watakaoumia zaidi ni wafanyabiashara wanaotoa huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria kwa masafa makubwa.
Bajeti ya kihistoria Naye Askofu Bundala alisema binafsi yake anaona tangu uhuru haijawahi kutokea bajeti ya kisomi, ambayo ina malengo ya kuboresha maisha ya Watanzania kama ya mwaka huu wa 2017/18.
“Hii inaonesha ni jinsi gani sasa serikali yetu ilivyo kwa sasa hivi chini ya uongozi wa awamu ya tano, ilivyodhamiria katika kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na hali ya uchumi uliopo na hatimaye kumwezesha kumudu katika maisha yake ya kila siku,” alisema.
Kuhusu suala la vinywaji vikali kuongezewa kodi, Askofu huyo aliitaka serikali kuendelea kupandisha zaidi ili kupunguza hali ya ulevi nchini ulivyo, kwa kuwa hali hiyo husababisha watu kutofanya kazi kwa weledi na pia baadhi ya ajali husababishwa na ulevi.
Mrema: Mahabusu zitapumua Akizungumzia bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Mrema alisema bajeti ya mwaka mpya itapunguza ongezeko la wafungwa katika magereza na mahabusu kwa kuwa inawaelekeza watu katika kufanya shughuli halali za kuajiriwa na kujiajiri ili kupata kipato halali.
“Kwa kweli Rais Magufuli na Serikali yake watakuwa wametusaidia sana sisi tunaoshughulika na wafungwa maana hata wenye magari yaliyowekwa chini kwa kushindwa kulipia kodi, watayainua na kuyatumia kuongeza vipato yao.”
“Unajua uchumi au mazingira ya kufanya kazi halali yakiwa magumu, watu wanashindwa, wanakwenda kufanya njia hatari za uhalifu, lakini sasa watasingizia nini. Hakuna atakayeona haja ya kujihusisha na uhalifu ndiyo maana nasema magereza zitapumua,” alisema.
Akaongeza, “Hata kitendo cha kuondoa kodi ya mwaka katika leseni la magari na kusamehe madeni ya malimbikizo, na kuondoa kodi kwa usafirishaji mazao wilaya hadi wilaya chini ya tani moja karibu magunia 20, kitavutia wengi kufanya shughuli halali.”
Mrema akaenda mbali na kusema, “Wengine walisema atafukuza wawekezaji na pesa zimepotea, haya sasa kuna mazingira ya hela yamefunguliwa kila kona; watu wampe muda rais atengeneze na kuinyoosha nchi.”
Wabunge waipokea kwa nderemo Wabunge wengi bila kujali tofauti za vyama vyao, wamesifia bajeti hiyo ya serikali ya mwaka 2017/2018, kwa kufuta ushuru ambao ni kero kwa wananchi.
Walisema hayo walipohojiwa mjini hapa juzi, ambapo Mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama (CCM) alisema bajeti hiyo ni ya kumjali mwananchi kutokana na kuondolewa kwa tozo hasa ushuru wa magari.
Alisema kuondolewa kwa ushuru huo, kutawafanya watu wengi wenye magari, wafanye kazi zaidi na malori yabebe chakula kingi zaidi. “Kinachotakiwa ni namna ya kusimamia bajeti hiyo ili iweze kutekelezwa na wananchi wakaona faida yake tangu Julai mosi, mwaka huu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati (CCM) alisema ada ya leseni ilikuwa ikichangia kuleta adha kwa watumiaji wa magari. Alisema mbaya zaidi wamiliki wa magari, hata kama hayapo barabarani, walikuwa wakitozwa ada hiyo na kutozwa faini, hivyo kitendo cha kufuta kodi hiyo kitapunguza adha hiyo.
“Lakini pia kitendo cha serikali kufuta kodi ya mazao kitawapa mwanya watu wengi kusafirisha mazao yao badala ya mfumo wa sasa ambao walikuwa wakitozwa hata mazao kidogo,” alisema. Mbunge wa Viti Maalumu, Matha Mlata (CCM) alisema kuondoa ada ya leseni barabarani, kutaleta unafuu katika biashara kwa wananchi.
Alisema kufuta kodi mbalimbali kwenye mazao ya wakulima, kutaongeza kasi katika uzalishaji kwenye kilimo kwani kodi hizo zilikuwa zikisumbua wananchi. Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM) alisema kuondoa ada kwenye usajili wa magari, kutapunguza adha kubwa na serikali ilikuwa ikipoteza fedha kutokana na watu wengi kutolipa.
Alisema kitendo cha kuondoa kodi katika mazao, kitaongeza uzalishaji na wananchi wengi wataongeza uzalishaji. Alisema lakini kuongeza kodi katika mazao au bidhaa kutoka nje, kutakuza viwanda kutokana na wananchi wengi watajikita katika kuzalisha zaidi.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) alisema ni tendo jema kufuta ada ya magari ambayo yalikuwa hayafanyi kazi, lakini alisema kupeleka kwenye mafuta ni kuongeza mzigo kwa wananchi.
“Kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari ni jambo jema, lakini kwa kuongeza kwenye mafuta ni kuongeza mzigo kwa watumiaji,” alisema na kuongeza: “Mzigo huo utawaelemea wananchi kwani watatakiwa kulipia mafuta wanayonunua kwa ajili ya jenereta, vibatari, mashine za kusaga na mashine nyingine,” alisema.
Alisema bajeti bado ni tegemezi kwamba inategemea wafadhili kwa asilimia 11, ambao wamekuwa hawatoi fedha jambo zinawekwa kwenye bajeti. Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) alisema pamoja na kufuta kodi hizo, bado bajeti hiyo ni tegemezi kutokana na kuwa inategemea asilimia 37 ya fedha za nje ikiwamo mikopo, misaada na washirika wa maendeleo.
Alisema bajeti hiyo inategemea fedha za nje kwa zaidi ya Sh trilioni 11, kitendo ambacho hakipendezi. Alisema kwa miaka mingi bajeti hiyo imekuwa ikipandisha bei za juisi, soda, bia, sigara, hivyo ingekuwa vema kutafuta vyanzo vingine.
Akiwasilisha bajeti ya serikali bungeni juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema serikali imefuta ada ya mwaka ya leseni ya magari ili ada hiyo ilipwe mara moja tu gari linaposajiliwa ; na baada ya hapo iendelee kulipwa kupitia ushuru wa bidhaa za mafuta ya petrol na dizeli Dk Mpango alisema serikali inatoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote ya ada hiyo, yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma.
Muleba wafurahia bajeti Wananchi wilayani Muleba, mkoani Kagera wameeleza kufurahishwa na hatua zilizotangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
Salome Bin’Omugabi (30), mfanyabiashara anayemiliki duka la rejareja wilayani Muleba, alisema amefarijika na tamko la Serikali la kukemea maofisa wa Mamlaka Mapato Nchini (TRA), wasio waaminifu na ambao wamekuwa wakisababisha kero kwa wafanyabiashara.
Alisema wajibu wa kulipa kodi ni jukumu la kila Mtanzania, na kuongeza kuwa kinachohitajika ni mazingira mazuri ya kufanyia biashara. Hassan Tirukaizire (25) mjasiriamali mkazi wa mji mdogo wa Kamachumu wilayani Muleba, alisema amekuwa akisafirisha mikungu miwili ya ndizi kutoka Buganguzi na kuipeleka katika Bandari ya Kemondo, lakini amekuwa akikumbana na vizuizi, hasa katika eneo la Kanyinya.
Alidai kuwa askari mgambo walikuwa wakimdai awapatie Sh 2,000 kwa kila mkungu wa ndizi, hata pale alipokuwa bado hajafikisha ndizi zake na kuziuza Kemondo. Mpango alitangaza kuwa Serikali imeondoa Ushuru kwa wasafirishaji wa mazao ya chakula chini ya tani moja kutoka halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine.
Aidha, Mpango alitangaza kuwa ushuru wa mazao umepungua kutoka asilimia tano hadi tatu kwa mazao ya biashara.

Tupia Comments: