KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu amewataka wanachama wa CCM Tawi la Chukwani kutumia vizuri fursa ya Uchaguzi wa Chama kuwachagua viongozi na watendaji waadilifu na wasioyumbishwa wakati wanapotekeleza majukumu.
Rai hiyo aliitoa wakati akizungumza na wanachama na Kamati ya siasa ya Tawi la Chukwani katika ziara ya kuimarisha chama huko katika Ofisi ya Tawi la Chukwani nje kidogo ya Mjini wa Zanzibar.
Alisema safu za viongozi wa ngazi mbali mbali watakaochaguliwa kupitia uchaguzi huo ndio watakaokuwa na jukumu la kuwaidhinisha viongozi watakaovusha chama hicho salama na kuhakikisha kinashinda kwa ngazi zote katika uchaguzi mkuu ujao.
Kupitia kikao hicho aliwaagiza Viongozi wa ngazi ya majimbo ambao ni Mbunge, Mwakilishi na Madiwani kuhakikisha wanasilisha kwa wananchi wao taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020 ili waweze kujua ahadi zilizotekelezwa na kuhoji ambazo bado utekelezaji wake.
Alisema Katiba ya Chama hicho inaagiza Viongozi hao kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Ilani kila baada ya miezi mitatu kwa wananchi pamoja na ngazi za juu za chama ili waweze kujiridhisha kama ahadi zilizoahidiwa wakati wa kampeni kama zimetekelezwa kwa ufanisi.
Pamoja na agizo hilo pia aliwataka viongozi hao kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu na wahusika.
“ Viongozi lazima tuendeleze utamaduni wa kuwa karibu zaidi na wananchi wetu kwani ndio waliotuajiri katika nafasi hizi tulizokuwa nazo na mkataba wetu na wao ni kuwatatulia kero zinazowakabili katika maeneo yao.
Pia naamini mnatekeleza ilani ya Uchaguzi lakini kama hamrudi kwa wananchi mkawambia mliyoyafanya wakafahamu mnatarajia wao watajuaje kama kuna ahadi zimetekelezwa katika jimbo husika, lazima tubadilike na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.”, alisema Waride na kuongeza kwamba msimamo wa CCM ni kujiimarisha kuanzia ngazi za chini wadi na matawi.
Pamoja na hayo alisema njia pakee ya kumaliza baadhi ya malalamiko katika Tawi hilo ni viongozi na wanachama kutumia njia ya vikao rasmi vya Kikatiba kujadili changamoto zinazowakabili ili waweze kupata maamuzi ya pamoja ya kutafuta ufumbuzi wake.
Naye Kaimu Katibu wa Tawi hilo, Iddi Khamis Akitoa tathmini ya Uchaguzi wa CCM kwa ngazi ya Tawi na jumuiya alisema linaendelea vizuri na kwa baadhi ya ngazi tayari fomu zote zimepata wagombea wa nafasi za uongozi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mwanaasha Khamis Juma alisema toka ameshika nafasi ya uongozi ameshiriki kikamilifu kutatua changamoto za jimbo hilo zikiwemo kufanikisha upatikanaji wa maji safi na salama, kusaidia vikundi vya ujasiria mali kwa wanawake na vijana na kuahidi kuendelea kuzitafutia ufumbuzi hatua kwa hatua kero zingine zilizipo katika jimbo hilo.
Wakizungumza baadhi ya wanachama wa Tawi hilo waliwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama hicho kwa wanannchi wote.
Pia walilalamikia changamoto ya uongozi wa Tawi hilo kutofanya vikao vya kikanuni mara kwa mara hali inayosababisha baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kutotekeleza wajibu wao ipasavyo.
Tupia Comments: