KAULI ya Rais John Magufuli aliyoitoa akihutubia sherehe za Mei Mosi mwaka huu ya kuwachukulia hatua wazee ambao wamerudisha nyuma umri, imepokewa kwa hisia tofauti wakiwemo wasomi.
Kwa mtazamao wangu, naona wengi wanaunga mkono walioghushi vyeti wachukuliwe hatua za kisheria huku wengine wakihitaji wenye taarifa zenye mkanganyiko kutokana na wazazi wao kutokujua kwa hakika umri wao, watizamwe kwa jicho la tofauti.
Baadhi ya wasomi hao wanasema ikiwa mtumishi ana vyeti viwili vya kuzaliwa, vikionesha miaka tofauti ya kuzaliwa, na amezaliwa miaka 45 iliyopita, huyo anakosa la jinai na anapaswa kuchukuliwa hatua bila kuonewa huruma.
Wanasema kama mtu ana vyeti vimetolewa na mamlaka husika ya vyeti vikiwa na taarifa mbili tofauti na amezaliwa miaka ya kuanzia 1970, huyu achukuliwe hatua. Nilizungumza na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mkombozi Mhina ambaye kwa upande wake anasema kama mtu aliajiriwa akaandika taarifa zake, ni yeye anayepaswa kuthibitisha umri wake au wazazi wake ambao nao wengi hawajui miaka waliyowazaa watoto wao.
Pia nilihojiana na Katibu wa Chama cha Mawasiliano na Mtandao wa Simu (Tewuta), Junus Ndaro alisema ni kweli kuna watu wengi kwenye ofisi za serikali ambao wana umri zaidi ya miaka 60 kwa sababu wengi walibadilisha umri miaka ya nyuma baada ya kuwepo sheria ya kustaafu ukiwa na miaka 55.
Anasema wengi waliona sheria hiyo inawafanya wastaafu wangali vijana, kwa hiyo kwa kuwa wengi hawana vyeti vya kuzaliwa walibadilisha taarifa zao kirahisi ili waweze kustaafu wakiwa na umri mkubwa.
Hata hivyo, baada ya umri wa kustaafu kuongezwa kutoka miaka 55 hadi 60, serikali kupitia Ofisi ya Utumishi ilitoa waraka kuwataka watumishi wote wasibadilishe umri wao waliouandikisha.
Anasema zuio hilo lilifanya watumishi wengi ambao walikuwa wamebadilisha umri washindwe kwenda kubadilisha taarifa zao, licha ya kuwa wapo watumishi wengi ambao ni wazee wangependa kustaafu lakini waraka huo uliwabana.
Akaongeza kwamba kuna watu anaowafahamu ambao waliomba wabadilishe taarifa zao, lakini mwajiri aliwazuia kutokana na waraka huo wa Utumishi. Alisema Utumishi ilitoa waraka huo kwa kuamini kuwa wakati mtumishi alipokuwa anajaza taarifa zake alikuwa kijana na alikuwa na akili timamu.
Pia nilizungumza na Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Vyama ya Wafanyakazi (TUCTA), Nestory Ngulla ambaye yeye anasema wazee wengi bado wako kwenye utumishi wa umma kwa sababu wengi wao hawajui hata tarehe walizozaliwa kutokana na wazazi wao kutokuwa na ufahamu wa kutambua miaka.
Akatolea mfano yeye mwenyewe kwamba alikuja kutambua umri wake baada ya kupelekwa shule kuanza darasa la kwanza akaelezwa na walimu kuwa amezaliwa mwaka 1946. Lakini mwezi na tarehe alibuni mwenyewe kwa sababu mama yake hakuwa anafahamu ila alikuwa anasema tu alimzaa wakati wa mvua nyingi.
Kwa hiyo, ni vema mamlaka zikatazama vizazi na kuanza kuhakiki vyeti vya umri kuanzia miaka ya 1970, kwa kuwa miaka ya nyuma, wengi walikadiriwa miaka kutokana na mazingira na matukio.

Tupia Comments: