Großbritannien Manchester - Trauer nach Terroranschlag (Getty Images/L. Neal)
Watu wakiweka maua katika eneo la shambulio mjini Manchester
Polisi ya Uingereza  imesitisha kubadilishana taarifa za siri na Marekani zinazohusu shambulio la bomu la kujitoa muhanga mjini Manchester, limeripoti shirika la habari la BBC leo.
Hatua  hiyo  ni kwasababu ya hofu ya kuvuja kwa  taarifa hizo katika vyombo vya habari nchini Marekani ambako kunaweza kuzuwia msako wa kumtafuta  mtu ambaye huenda  amehusika  katika  utengenezaji  wa  bomu ambaye hadi  sasa hajapatikana.
Iwapo itathibitishwa , hatua  hiyo  ya  kuzuwia  kupeana  taarifa  na mshirika  muhimu  kabisa  wa  Uingereza  katika  ulinzi na  usalama kutaonesha  kiwango cha  hasira  ya  Uingereza  kuhusiana  na kuvuja  katika  vyombo  vya  habari  nchini  Marekani  kuhusu  taarifa za  uchunguzi  wa  polisi.
UK | Trauerbekundungen nach dem Anschlag in Manchester (picture-alliance/empics/B. Birchall)
wakaazi wa Machenster wakitoa rambi rambi zao katika eneo la tukio
Waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa  May  atalizusha  suala  hilo wakati wa  mkutano wake  na  rais  wa  Marekani  Donald Trump leo, vyanzo  katika  serikali  vimelieleza  shirika  la  habari  la Reuters, baada  ya  gazeti  la  New York Times  kuchapisha  picha za  eneo  lililotokea  mashambulizi  mjini  Manchester  ambako watu 22 waliuwawa.
Picha  hizo  ni  pamoja  na  mabaki  ya  bomu  linaloshukiwa kutumiwa katika  shambulio  hilo, mfuko  wa  kubeba  mgongoni uliokuwa  umebebwa  na  mshambuliaji  wa  kujitoa  muhanga na kuonesha  damu  katika mabaki  ya  magari  yaliyoharibiwa.
Kuvuja  kwa  taarifa
Shirika  la  utangazaji  la  BBC  limesema  polisi  ya  Manchester inamatumaini  ya  kurejesha  uhusiano  wa  kupashana  habari  za kijasusi  hivi  karibuni  lakini  kwa  sasa  imekasirishwa.
Großbritannien - Mutmaßlicher Attentäter in Manchester von Überwachungskamera gesehen (picture-alliance/AP Photo/Sky News)
Picha ya mshambuliaji Salman Abedi kabla ya kujiripua
Baada  ya  shambulio  baya  kabisa  kuwahi kuwauwa  watu nchini Uingereza   tangu  mwaka  2005, polisi  imo  katika  msako kumtafuta  mshirika  ambae  inashuku  alimsaidia  Salman Abedi kutengeneza  bomu  hilo  lililowauwa  watu  22  siku  ya  Jumatatu katika ukumbi  wa  tamasha  la  muziki  uliojaa  watu  kaskazini  mwa mji nchini  Uingereza  wa  manchester.
Salman Abedi , mshambuliaji  wa  kujitoa  muhanga raia  wa Uingereza  , alikuwa  nchini  Ujerumani siku  nne  kabla  ya shambulio  hilo  siku  ya  Jumatatu, limeripoti  shirika  la  habari  la Sky , likinukuu  taarifa  za  kijasusi  za  Ujerumani.  Abedi  alikuwa katika  mji  wa  Dusseldorf , ambao  uko  kilometa  300 magharibi mwa  mji  mkuu  Berlin.
Uhusiano na mshambuliaji
Wachunguzi  wanaonesha  kwamba  Abedi alikuwa  sehemu  ya  mtandao mpana  wa  wanamgambo. Kile  kinachowapa  hofu  majirani wa Abedi  hivi  sasa  ni uhusiano  ambao  haujulikani  kati  ya mshambuliaji  na  ndugu  zake ambao ni  washukiwa  na  kati ya shambulio  hilo  na  imani  yake.  Wakati  baba  yake  Abedi  na ndugu  zake  wanashikiliwa  kwa  ajili  ya  uchunguzi , waandishi habari  wamekwenda  katika  msikiti  mkubwa  mjini  Manchester kutaka  kujua ushahidi  wa  kuhusika katika  shambulio  hilo. Mfanyakazi  mmoja  wa  msikiti  huo  amesema:
Großbritannien Manchester Gedenken (DW/L. Bevanger)
Imam Yusuf Chunara wa msikiti wa Manchester
"Sifurahii  kabisa kwa  kweli, kwasababu  kwa  sehemu  fulani wanahusisha  tukio  hili  na  Uislamu. Huu  sio Uislamu, Haiwakilishi Uislamu. Sidhani  wanapaswa  kuwa  hapa."
Großbritannien PK Theresa May zum Anschlag in Manchester (Reuters/T. Melville)
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa  May  atasimamia  kikao cha kamati  ya  serikali  inayochukua  hatua  za  dharura  leo , amesema msemaji  wa  ofisi  yake. May  ambae  anatarajiwa  kwenda  mjini Brussels  baadaye  leo  kwa  ajili  ya  mkutano  wa  jumuiya  ya NATO  amekuwa  na  mikutano  kadhaa  ya  kamati  hiyo  tangu shambulio  hilo  kufanyika  siku  ya  Jumatatu.

Tupia Comments: