Ikiwa imepita siku mbili tangu Rais John Magufuli kueleza kuwa kwa sasa nchi iko katika vita ya uchumi na kwamba ana majina ya watu waliotaka kuingilia na kuharibu uchunguzi wa Kamati Maalumu aliyoiunda ili kuchunguza thamani na viwango vya madini vilivyomo kwenye mchanga wenye madini (Makinikia) katika makontena 277 yaliyozuiliwa kusafirishwa nje ya nchi, ili kupoteza ushahidi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole Mei 25, 2017 aliibuka na kudai kuwa kuna wahujumu uchumi walitaka kumhonga kiasi cha Bilioni 300 Rais Magufuli, ili kusitisha zoezi la uchunguzi huo, huku akihoji masilahi wanayopata watu wanaofanya biashara ya kusafirisha makinikia hayo nje ya nchi.
“Vita ziko za aina nyingi, ziko zile tunazopigana kwa silaha mtu na mtu, na nchi na nchi, lakini sasa ziko vita za kiuchumi, ni mbaya zaidi zinalenga kuturudisha nyuma.Wahujumu uchumi hawapigani na rais, bali wanapigana na maisha ya wananchi wa Tanzania, tukiwa wamoja tutashinda vita hii, wako watu wanaipinga vita hii yenye dhamira njema, huu si wakati wa kutofautiana ni wakati wa kusimama kumshinda adui,”alisema.
Polepole aliyasema hayo, wakati akitoa wito kwa wananchi, kumuunga mkono Rais Magufuli katika kipindi hiki kigumu kwani nchi iko katika vita mbaya ya uchumi ambayo wahujumu uchumi wamelenga kupigana na maisha ya watanzania na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.
“Kuna watu walitaka kumhonga rais bilioni 300 ili kusitisha uchunguzi. Walitaka kuhonga bilioni 300 kwa ajili ya kusitisha uchunguzi huo, hivi wao wanapata fedha kiasi gani? Lakini rais akawatolea nje, akasema subirini uchunguzi ukamilike. Tusiamame naye na hakika tutashinda na historia itaandikwa kwamba tulisimama katika kulinda urithi wetu,”amesema.
Katika hatua nyingine, Polepole aliwajibu baadhi ya wanansiasa wanaoikosoa CCM kutokana na viongozi wake waliopita kutunga na kupitisha sheria za madini ambazo zinatetea masilahi ya wawekezaji kuliko nchi, kwa kusema kuwa viongozi walioko sasa ni tofauti na waliopita, na kwamba serikali iliyoko madaraka itarekebisha sheria hizo.
“Tumehujumiwa sana, tumedhurumiwa sana mali za watanzania ambazo tumezirithi kutoka kwa mababu zetu na tuna dhamana ya kuhakikisha zinawafikia watoto wa watoto wetu,” alisema.
Tupia Comments: