Viongozi wa mataifa saba tajiri duniani wanakutana na viongozi wa mataifa ya Afrika Jumamosi(27.05.2017)siku ya mwisho ya mkutano wao wa kila mwaka ambao umegubikwa na kutokukubaliana kuhusu mabadiliko ya tabia nchi,
Pamoja na hali hiyo ya kutokubaliana kuhusu mabadiliko ya tabia nchi , lakini umoja umepatikana katika kupambana na ugaidi.
Rais wa Marekani Donald Trump aliwaambia wenzake wa G7 kutoka Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani , Italia na Japan siku ya Ijumaa kwamba bado hajaamua iwapo kuendelea na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi wa kudhibiti utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira za kaboni.
Rais Donald Trump wa Marekani(kulia) na kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) katika mkutano wa G7 mjini Sicily, Italia
Viongozi wa Ulaya wameeleza kukatishwa kwao taama nje ya mkutano huo kwa kulazimika kurejea suala ambalo wanaamini limekwisha tiwa saini na kukamilika miaka miwili iliyopita.
Pia kulikuwa na msuguano unaoendelea kuhusiana na biashara ya dunia, pamoja na Trump, ambae alichaguliwa kwa ahdi ya kuiweka Marekani kwanza, akilaumu makubaliano ya kibiashara na makundi ya nchi kwamba yamesababisha nakisi katika biashara na Marekani na kudai kile alichoeleza kuwa ni "uwanja uliosawa " wa kushughulikia masuala ya biashara.
Hata hivyo , viongozi wa G7 wamesema kuna makubaliano makubwa kuhusiana na masuala kadhaa yanayobishaniwa ya sera za mambo ya kigeni , ikiwa ni pamoja na Syria , Libya na Korea kaskazini.
Taarifa za mitandao ya kijamii
Pia wameahidi kuongeza juhudi zao kupambana na itikali kali baada ya mwanamgambo wa Kiislamu kushambulia kwa bomu la kujitoa muhanga katika tamasha la muziki ambapo watu 22 waliuwawa kaskazini mwa Uingereza siku ya Jumatatu, na kuyaambia makampuni yanayotoa huduma ya internet na mitandao ya kijamii "kuongeza kwa kiasi kikubwa" juhudi zao za kuzuwia taarifa za wenye itikadi kali.
"Kitisho cha ugaidi ni suala moja ambalo nchi zetu zote zinakikabili na kwa sasa kuliko ilivyokuwa hapo kabla tunapaswa kuongeza nguvu zetu kukabiliana na kitisho hiki," amesema waziri mkuu wa Uingereza Theresa May , ambaye alishindwa kuhudhuria kikao cha jana Jumamosi na kurejea nyumbani siku moja mapema kwasababu ya shambulio hilo la Manchester.
Italia imekuwa mwenyeji wa mkutano huo wa G7 katika kisiwa cha Sicily kuvuta hisia kwa ajili ya Afrika na madhila ya wahamiaji ambao wanahatarisha maisha yao kwa idadi kubwa kwa kufanya safari hatari katika bahari ya Mediterania ili kutafuta maisha bora katika bara la Ulaya.
Wahamiaji wazidi kuingia Ulaya
Zaidi ya watu nusu milioni wameingia nchini Italia tangu mwaka 2014, wakati watu 1,400 walifikishwa katika fukwe na waokoaji siku ya Ijumaa pekee.
Viongozi wa Tunisia, Kenya, Ethiopia , Niger na Nigeria watajiunga na majadiliano leo asubuhi , ambapo Italia inataka mataifa hayo tajiri kabisa duniani kusaidia bara hilo kuendeleza uchumi wake katika juhudi za kuwashawishi vijana wa Kiafrika kubakia nyumbani.
Viongozi hao wanatarajiwa kutoa taarifa fupi ya pamoja kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita, ambapo mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya alidokeza kwamba huenda ikawa ya kurasa sita tu ikilinganishwa na kurasa 32 mwaka jana
Tupia Comments: