SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea na utaratibu wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi mwaka hadi mwaka ili waweze kumudu hali ya maisha.
Hayo yalisemwa jana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akiwahutubia wananchi katika kilele cha sherehe ya Siku ya Wafanyakazi duniani zilizofanyika Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema anafahamu umuhimu wa watumishi na wajibu wao na ndiyo sababu amechukua hatua ya kupandisha mishahara na posho mbali mbali kadri hali ya uchumi na ukusanyaji wa mapato inavyoruhusu.
”Katika kipinidi cha kwanza cha uongozi wangu, nilipandisha mishahara mara tatu, mwaka 2011, 2013 na 2015…vilevile wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, niliahidi tena kuwa Serikali nitakayoingoza katika kipindi cha pili mwaka 2015-2020 itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta ya umma kwa asilimia 100 kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 300,000,’’ alisema.
Aidha, alisema anajua katika utekelezaji wa mchakato wa nyongeza za mishahara, hujitokeza malalamiko na changamato kadhaa ambazo huhitaji kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa umakini ili zisiathiri malengo ya Serikali ya kuwapa ari, hamasa na hamu watumishi kutekeleza wajibu wao.
Alisema Serikali itazishughulikia changamoto zote zitakazojitokeza kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na zitapatiwa ufumbuzi haraka.
Alisema pia Serikali imeimarisha mazingira ya kazi, kuziimarisha sheria za kazi, kurekebisha mishahara kwa kutegemea viwango vya taaluma, kurekebisha mishahara kwa kutegemea uzoefu wa mfanyakazi, utaratibu kwa wanaokwenda likizo na kuwalipa posho wanayostahili.
Aisema baadhi ya watumishi wamekuwa na dharau kwa wananchi wanapokwenda kutaka huduma na wengine huwataka watoe rushwa ndipo wahudumiwe.
”Niliahidi kuwa Serikali itawashughulikia watumishi wa namna hii. Katika kipindi cha mwaka uliopita tulianza kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi hao, lakini bado wapo ambao hawajajirekebisha,’’ alisema.
Alisema serikali haitawavumilia wote wenye tabia ya kutoroka kazini, kuchelewa, wasiojali kanuni za utumishi wa umma, wababaishaji na wasiojali na wanaojifanya wababe
Tupia Comments: