Kansela Angela Merkel na Rais Vladimir Putin (Picha ya Maktaba)
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin katika mji wa Sochi nchini Urusi. Mazungumzo yao yatajikita katika migogoro ya Syria na Ukraine, na pia maandalizi ya mkutano wa G20.
Hii ni ziara ya kwanza ya Kansela Angela Merkel nchini Urusi kwa muda wa miaka miwili, na hiyo inaashiria kurejea kwa mjadala kati ya nchi hizo, baada ya tofauti za muda mrefu ambazo kwa kiasi kikubwa zina msingi katika mzozo wa Ukraine. Hatua ya Urusi kulichukua kimabavu eneo la Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014, na kuunga mkono waasi wa mashariki mwa nchi hiyo wanaotaka kujitenga, vimemfanya Kansela Merkel kuunga mkono vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi. Urusi nayo ilijibu vikwazo hivyo kwa kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka nchi za Magharibi.
Bi Merkel anakwenda Urusi kufuatia wito wa Rais Vladimir Putin alioutoa wakati wa ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel mjini Moscow, akitaka mahusiano baina ya nchi yake na Ujerumani kurejeshwa katika hali ya kawaida.
Miaka miwili ya mkwamo
Ukraine Checkpoint in Luhansk (Getty Images/AFP/A. Filippov)
Vita Mashariki mwa Ukraine vimekuwa kikwazo katika uhusiano kati ya Ujerumani na Urusi
Tangu ziara ya mwisho ya Kansela Merkel nchini Urusi mwezi Mei 2015, mawasiliano baina yake na Rais Vladimir Putin yamekuwa yakipitia katika mikutano ya pande nne, iliyowashirikisha pia marais Francois Hollande wa Ufaransa na Petro Poroshenko wa Ukraine, kuhusiana na mgogoro wa Ukraine.
Msemaji wa Kansela Merkel Steffen Seibert amesema lengo la Ujerumani ni kujaribu kuileta Urusi  katika mchakato wa kutafuta makubaliano yenye tija, katika mzozo wa Ukraine ambao ameutaja kama 'kigezo kigumu' kisichoweza kupuuzwa. Kitu kingine muhimu kisichoweza kupuuzwa, ni ushawishi wa Urusi katika migogoro mikubwa inayoendelea duniani, yaani Ukraine na Syria, ambayo hakuna suluhisho linaloweza kupatikana bila kusihirikisha serikali ya mjini Moscow.
Maandalizi ya mkutano wa G20 pia ni mada muhimu
Deutschland G20-Vorbereitungen in Hamburg - Elbphilharmonie (DW/A. Drechsel)
Mji wa Hamburg utakaopokea mkutano wa kilele wa G20 Julai, 2017
Mkutano baina ya Merkel na Putin unafanyika siku chache tu baada ya kuuawa kwa muangalizi wa Shirika la Ulaya kuhusu Usalama na Ushirikiano OSCE. Mwangalizi huyo aliuawa na bomu la kutegwa ardhini katika jimbo la Luhansk, mojawapo ya majimbo mawili ambayo waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanataka kuyatenga kutoka Ukraine.
Mkutano wa kilele wa nchi tajiri duniani na zinazoinukia kiuchumi, maarufu kama G20 utakaofanyika mjini Hamburg hapa Ujerumani kuanzia tarehe 7-8 Julai mwaka huu utakuwa mada nyingine muhimu katika mazungumzo kati ya Kansela Merkel na Putin, ikizingatiwa kuwa mkutano huo umekuwa njia pekee aliyo nayo rais Putin kukutana na viongozi wengine muhimu duniani.

Tupia Comments: