Mkewe rais wa Nigeria Aisha Buhari amesema kuwa mumewe sio mgonjwa sana zaidi ya inavyodhaniwa.
Alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter akisema kuwa Muhammadu Buhari mwenye umri wa miaka 74 anaendelea na majukumu yake na kwamba amekuwa akikutana na mawaziri.
Kundi moja la watu mashuhuri lilimtaka rais Buhari kuchukua likizo ya matibabu kufuatia wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya.
Mnamo mwezi Machi alirudi nchini Nigeria baada ya likizo ya matibabu iliochukuwa wiki saba nchini Uingereza ambapo alitibiwa ugonjwa usiojulikana.
- Je Aisha Buhari ni nani?
- Buhari: Mke wangu ni wa kwangu jikoni
- Buhari apewa onyo kali na mkewe Nigeria
Wakati aliporudi nyumbani alisema kuwa hajawahi kuwa mgonjwa sana maishani mwake.
Rais huyo hajaonekana hadharani kwa kipindi cha wiki moja sasa, na hatua ya kutohudhuria mkutano wa baraza la mawaziri pamoja na ibada ya kila wiki ya Waislamu inayofanyika siku ya Ijumaa, imesababisha uvumi zaidi kuhusu hali yake ya kiafya, kundi hilo la watu 13 limesema katika taarifa.
Bi Buhari alishutumiwa na mumewe mwaka uliopita aliposema katika mahojiano ya BBC kwamba hataunga mkono kuchaguliwa tena kwa mumewe hadi pale atakapofanya mabadiliko katika serikali yake akidai kuwa imetekwa na watu wachache.
Na akijibu matamshi hayo ya mkewe bwana Buhari alisema kwamba mkewe anafaa kuwa katika chumba chengine
Aisha Buhari akimkarisha nyumbani mumewe baada ya kuwasili kutoka kwa likizo ya matibabu nchini Uingereza
Waziri wa habari Lai Mohammed aliambia BBC kwamba afya ya rais ni swala la kibinafsi na kwamba raia wa Nigeria wamekuwa wakielezwa kuhusu hali yake.
Kundi hilo linashirikisha wanaharakati wenye ushawishi mkubwa akiwemo wakili Femi Falana, mchanganuzi wa maswala ya kisiasa Jibrin Ibrahim na kiongozi wa shirika la Transparence International tawi la Nigeria Anwal Musa Rafsanjani.
Raia hao 13 wanasema kuwa walilazimika kumshauri rais Buhari kusikiza ushauri wa daktari wake wa kibinafsi kwa kuchukua mapumziko ili kuangazia afya yake bila kuchelewa.
Msaidizi wa Bwana Buhari ,Bashir Ahmed alisema kuwa rais alikutana na waziri wa haki Abubakr Malami na maafisa wengine katika jumba la rais siku ya Jumanne ikiwa miongoni mwa majukumu yake.
Wiki iliopita, msemaji wa rais Garba Shehu alisema kuwa bwana Buhari alikuwa akichukua majukumu yake polepole huku akiendelea kupona kufuatia kipindi kirefu cha matibabu nchini Uingereza.
Tupia Comments: