Dhana kwamba Rais wa Marekani Donald Trump ametumia vibaya madaraka yake zinahanikiza. Kiongozi wa zamani wa shirika la upelelezi la FBI Robert Mueller achunguza kama Urusi imeshawishi uchaguzi wa Marekani mwaka jana.
Alikuwa Rod Rosenstein wa wizara ya sheria aliyetangaza kuteuliwa Robert Muelller, aliyewahi kuliongoza shirika la upelelezi la Marekani FBI kuanzia utawala wa George W. Bush na baadae katika utawala wa Barack Obama.
Uamuzi huo umefuatia wiki ya zahma ailiyopiga ikulu ya White House baada ya rais Donald Trump kumwachisha kazi mkurugenzi wa shirika la FBI James Comey. Wademocrats na baadhi ya wafuasi wa chama cha Republican walipaza sauti kudai iundwe tume huru kuchunguza kama Urusi ilijaribu kwa njia moja au nyengine kushawishi matokeo ya uchaguzi wa rais Novemba mwaka jana.
Rais Trump ,anaeendelea kulalamika kwamba vyombo vya habari vinamwaandama, amejibu kijuu tuu ripoti kuhusu kuteuliwa mkurugenzi huyo wa zamani wa FBI, anaeheshimiwa kupita kiasi na kusema, "uchunguzi kamili utathibitisha kile ambacho tayari tunakijua" hakuna njama yoyote kati ya washauri wangu wa kampeni na nchi yoyote ya kigeni", amesema rais Trump na kuongeza "Nna pupa kuona kadhia hiyo inakikamilishwa haraka.
Uamuzi wa kuteuliwa Robert Müller ni pigo kwa ikulu ya Marekani
Kimsingi Robert Mueller atakuwa huru kuendesha shughuli zake kuliko kwa mfano mwendesha mashitaka mkuu au hata mkurugenzi mkuu wa shirika la upelelezi la FBI. Na zaidi ya hayo hakuna anaeweza kumfukuza kazi. Katika tukio ambalo ni nadra kushuhudiwa, safari hii wademocrat na warepublican wamesifu kuteuliwa kwake.
Wabunge wa chama cha democrats katika mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani-Congress wanasherehekea ushindi ingawa kuna wanaohisi hii ni hatua ya mwanzo tu wakitilia mkazo iundwe tume maalum kushughulikia suala la Urusi, tume itakayokuwa na madaraka makubwa zaidi kuliko kufanya uchunguzi.
Zahma zinazopiga White House zinayatikisa pia masoko ya hisa
Wakati huo huo tume ya masuala ya sheria ya baraza la Seneti imemwaalika mkurugenzi wa zamani wa shirika la upelelezi FBI James Comey akaelezea mambo yaliyotokea na kusababisha kufukuzwa kwake kazini. Hata hivyo James Comey hajaitika bado mwaliko huo.
Wasi wasi kuhusu dhana kwamba pengine rais Trump anatumia vibaya madaraka yake unayatikisa pia masoko ya hisa . Wall Street imefunga kwa kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu Novemba mwaka jana. Huku soko la hisa la Tokyo nchini Japan likiporomoka kwa asili mia 1.32, kufuatia sarafu ya Marekani Dollar kupoteza thamani yake.
Tupia Comments: