SAFARI ya Yanga katika michuano ya Afrika leo imefikia tamati baada ya kufungwa mabao 4-0 na Mouloudia Club Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Al-Jaza’ir, Algiers, Algeria katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Kwa matokeo hayo, Yanga inatolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam wiki iliyopita, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Guinea, Yakhouba Keita aliyesaidiwa na Aboubacar Doumbouya na Mamady Tere, hadi mapumziko, wenyeji walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Derraya Warid alimsetia Awady Said dakika ya 14 kuifungia MC Alger bao la kwanza dakika ya 14 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20 dakika ya 39.
Katika kipindi hicho, Yanga haikufanya shambulizi la maana langoni mwa MC Alger, wakati kipa wao, Deo Munish ‘Dida’ pamoja na kutunguliwa mara mbili, lakini pia aliokoa michomo miwili ya hatari.
Jahazi la Yanga lilizidi kuzama kipindi cha pili, baada ya Zerdab Zahir kuifungia MC Alger bao la tatu dakika ya 66 akitumia makosa ya mabeki wa Yanga kumuacha peke yake.
Na wakati refa Yakhouba Keita anajiandaa kupuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo huo, Awady Said akaifungia MC Alger bao la nne akitumia makosa ya mabeki wa Yanga, Kevin Yondan na Hassan Kessy kuchanganyana.
Dalili za Yanga kupoteza mchezo huo zilionekana mapema tu kutokana na kuibuka migogoro baina ya wachezaji na viongozi kabla ya safari ya Algeria mapema wiki hii.
Wachezaji wawili, beki Mtogo Vincent Bossou na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa waligoma kusafiri na timu kwa sababu ya madai ya mishahara yao ya miezi mitatu.
Na wachezaji waliondoka kwa ndege mbili tofauti Alhamisi mjini Dar es Salaam, kundi la kwanza likiondoka kwa ndege ya Emirates kupitia Dubai na kundi la pili likiondoka kwa ndege ya Uturuki kupitia Istanbul.
Kwa ujumla Yanga ilipatwa na mtikisiko wa kiuchumi tangu Februari, mwaka huu baada ya Mwenyekiti wake, Yussuf Manji ambaye pia ndiye mfadhili pekee wa timu kuingia matatizoni na Serikali.
Yanga iliangukia kwenye kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia katika hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao ya ugenini, kufuatia sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka.
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea kesho kama kilivyokwenda kwa ndege za Uturuki na Emirates.
Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Andrew Vincent ‘Dante’, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke/Amissi Tambwe dk46.
Tupia Comments: