Imeelezwa kuwa sababu kubwa inayochangia watoto kuendelea kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya kikatili katika maeneo ya kanda ya ziwa ni jamii kukosa elimu kuhusu haki za watoto pamoja na kukosekana kwa ushirikiano pale kesi zinazopelekwa katika vyombo vya sheria.
Hayo yamesemwa leo June 16,2017 na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Viwanja vya Shycom Mjini Shinyanga.
Matiro alisema tatizo kubwa linalotokea wakati wa kutetea haki za watoto wanapofanyiwa ukatili ni kukosekana kwa ushirikiano wa jamii na wazazi pale kesi inapofika katika vyombo vya sheria ikiwemo mahakamani hivyo kusababisha kesi nyingi kufutika matokeo yake watoto wanaendelea kunyanyasika.
“Naomba tuweke mkazo zaidi katika elimu kwa jamii kuhusu haki za watoto,jamii ikibadilika tunaweza kumaliza tatizo la unyanyasaji wa watoto,wazazi wakielimika watajitokeza katika vyombo vya sheria kutoa ushahidi kwa vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto wao”,alieleza Matiro.
“Haki za watoto zinadidimizwaa sana kanda ya ziwa hasa mkoani Shinyanga kutokana na jamii kukosa elimu na kung’ang’ania mila na desturi zinazomgandamiza mtoto hususani mtoto wa kike hivyo mashirika na serikali tushirikiane kubadilisha fikra za jamii,wananchi wajue haki za watoto na wazilinde”,aliongeza Matiro.
“Bado kuna mambo yanawanyima haki watoto,watoto wanabakwa,wanafukuzwa,wanalawitiwa na wengine hawapelekwi shule,yote haya yanatokea kwa sababu watu hawana udhubutu wa kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria”,alieleza.
Katika hatua nyingine aliwataka watoto kutambua haki zao na wawe wanashirikishwa katika mambo yanayowahusu badala ya wazazi pekee kujiamlia.
“Tunaposema haki ya mtoto tunataka kwanza watoto wazijue haki zao,haki ya kuthaminiwa,kupata elimu,malezi,kutambulika lakini pia kushirikishwa,yapo mambo yanafanyika katika jamii zetu yanafanywa kinyume na haki za watoto,jamii yetu inatakiwa kutambua na kuziheshimu haki za watoto”,alisema Matiro.
“Ni jukumu letu kumlinda mtoto,kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria na serikali lakini pia kwa kuwa watoto ni taifa la kesho,tunapaswa kuwafundisha stadi za kazi,kuwafundisha haki zao”,alisema Matiro.
Tupia Comments: