AFISA HABARI WA TFF, ALFRED LUCAS.

Ombi la Yanga la mechi yao ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons kusogezwa mbele, limegonga mwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatia juhudi za ziada za shirikisho hilo kuiwezesha kurejea nchini.

Kutokana na kuchelewa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki, Yanga iliomba kusogezewa mechi yao mbele ya Kombe la FA kwa vile wachezaji wao waliondoka kwa mafungu huko Algeria walikokwenda kucheza mechi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Katika mechi hiyo, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 4-1 kufuatia kukubali kichapo cha mabao 4-0 ikiwa ni baada ya kushinda kwa bao 1-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya awali.

Hata hivyo, Yanga ambayo ililazimika kurudi kwa mafungu, kundi la pili lilikwamaa kutokana na kuchelewa kuiwahi ndege, hivyo kuiomba TFF kusogeza mchezo wao huo mbele kwa kuwa walitarajia kundi la mwisho kurejea jijini Alhamisi.

Hata hivyo, TFF ilifanya juhudi kwa kuwasiliana na Shirika la Ndege la Emirates na hivyo kufanikiwa kupata nafasi kwa kundi la mwisho ambalo litawasili leo.

Akizungumza na Nipashe jana, Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema, ni kweli Yanga waliomba kusogezewa mbele mchezo wao kwa madai kwamba wamekosa usafi wa kurejea kwa wakati jijini Dar es Salaam kutoka Algeria.

"Lakini hilo halitawezekana tumewaambia mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya Prisons upo pale pale na tulichokifanya ni kushirikiana nao kupata usafiri wa kuwarejesha kwa wakati.

"Tumewasaidia kufanya 'booking' Shirika la Ndege la Emirates na kuhusu kulipa wanalipia tiketi wao wenyewe, hivyo watawasili mapema na kuiwahi mechi hiyo," alisema Lucas.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, aliliambia Nipashe kwa njia ya simu kutoka Algeria kuwa, wameshapata uhakika wa safari na kwamba wapo uwanja wa ndege tayari kwa kurejea nchini.

Tupia Comments: