WAKATI Serikali imetangaza orodha ya majina ya watumishi wa umma wenye vyeti feki, Halmashauri za Miji, Wilaya, Manispaa na Majiji zimeongoza kwa kuwa na wafanyakazi wenye vyeti bandia huku taasisi za umma zikifuatia.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais John Magufuli juzi kupokea vitabu vyenye orodha ya watumishi wa umma ambao wamebainika kuwa ama na vyeti pungufu, vyeti tata na vyeti vya kughushi kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki.
Hatua ya kufanyika kwa uhakiki huo ambayo ilitokana na agizo la Rais Magufuli inafanya sasa kuwepo kwa nafasi wazi za ajira 12,000 kwa watu wenye sifa ambao wangeweza kuajiriwa katika nafasi hizo lakini nafasi zao zikakosekana kutokana na kuajiriwa kwa watu wasio na sifa.
Idadi hiyo inatokana pia na kubainika kuwepo kwa vyeti tata 3,076. Kwa mujibu wa orodha hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk Laurean Ndumbaro, halmashauri zina idadi ya wafanyakazi 8,716, huku taasisi za umma zikiwa na jumla ya wafanyakazi 1,216.
Wakati halmashauri za Mikoa ya Dar es Salaam na Tanga zinaonekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi, mikoa ya Simiyu, Mbeya, Songwe, Shinyanga, Ruvuma, Tabora na Singida imekuwa na idadi ndogo zaidi ya wafanyakazi hao.
Kwa mantiki hiyo, kubainika kwa idadi kubwa kwa kiwango hicho cha watumishi wenye vyeti vya kughushi katika halmashauri hizo mbali ya kutoa nafasi mpya za ajira lakini pia kutaiwezesha serikali kupata mafanikio katika miradi ya maendeleo kwa kuajiri watendaji wenye sifa stahiki ambao watasimamia miradi kutokana na fedha zake nyingi kuelekezwa katika halmashauri hizo.
Ukiondoa halmashauri, vyuo vya elimu ya juu ambavyo ndio tegemeo katika kuzalisha wataalamu, baadhi yake vimebainika kuwa na idadi kubwa ya watumishi wenye vyeti bandia huku Chuo Kikuu cha Sokoine kikiongoza katika kundi hilo kikiwa na wafanyakazi 33.
Aidha kwa upande wa kundi hilo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimejidhihirisha kuegemea kwenye weledi kwa kiwango kikubwa baada ya kuwa na mfanyakazi mmoja tu aliyebainika kuwa na cheti bandia.
Ukiondoa vyuo hivyo, Chuo cha Utumishi wa Umma kimebainika kuwa na wafanyakazi 10, Chuo Kikuu cha Dodoma wafanyakazi watano, Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili wafanyakazi watano, huku Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam kikibainika kuwa na watumishi sita.
Kwa upande wa vyuo vya elimu ya juu, manufaa ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wake ni pamoja na kuviwezesha vyuo hivyo kupata wafanyakazi wakiwemo wahadhiri wenye sifa hatua itakayokuza kiwango cha elimu kwa wanafunzi ambao sasa watafundishwa na watu wenye sifa za elimu.
Aidha orodha hiyo imezitaja taasisi za umma zenye wafanyakazi wenye vyeti bandia ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo imebainika kuwa na wafanyakazi wanane, Mfuko wa Pensheni wa PPF wafanyakazi 16, Shirika la Ndege (ATCL) wafanyakazi 7, Shirika la Reli (TRL) wafanyakazi 24, Mamlaka ya Reli wafanyakazi 39 na Mamlaka ya Anga wafanyakazi 22.
Tupia Comments: