MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Profesa Idris Kikula amesema ujio wa Wizara za Serikali chuoni hapo haujaathiri utendaji wa chuo. Amesema anashangazwa na kauli za baadhi ya watu wanaobeza baadhi ya wizara za serikali kuwa na Ofisi Udom.
Alisema hayo juzi mjini hapa mbele ya Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa taarifa ya watumishi hewa na maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo hicho. Profesa Kikula alisema chuo hicho kina eneo kubwa kiasi cha hekta 6,000 na eneo lililoendelezwa ni nusu tu.
“Muingiliano kati ya shughuli za Wizara na za Chuo unaosemwa si wa uhalisia, yamesemwa mengi kuwa wafanyakazi wa serikali wamekuja kuna mwingiliano si kweli” alisema. Alisema ujio wa serikali umesaidia kuboreshwa kwa baadhi ya majengo ambayo yalikuwa hayatumiki wakati wote hali iliyokuwa ikisababisha kutokea kwa wizi wa samani mbalimbali ikiwemo milango.
Aidha profesa Kikula alisema Chuo hicho kilianzishwa Machi 5, 2007 na kuanza kazi Septemba 2007. Alisema wakati wa kuanzishwa kwake lengo lilikuwa ni kudahili wanafunzi si chini ya 40,000 na chuo kinaendeshwa kwa mfumo wa vyuo vya ndani ambavyo jumla viko saba.
Alisema mpaka sasa chuo kina wanafunzi 23,123 ambapo kati yao 22,112 ni shahada za awali na 1,051 shahada za juu. Alisema jumla ya programu 186 zinaendeshwa chuoni hapo na kufanya kuwa chuo kikuu cha kwanza chenye programu nyingi.
Alisema jumla ya wanafunzi 31,649 wameshahitimu katika mahafali saba ambayo tayari yamefanyika chuoni hapo kati ya 2010 hadi 2016. Pia alisema chuo kimeweza kusomesha watumishi 400 kwa kutumia mapato yake ya ndani na hivyo kupunguza gharama za kuajiri wataalamu wa kigeni.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili ni kudaiwa kodi ya ardhi hekta 6,000 ambapo kodi yake ni Sh. Bilioni mbili ambazo ni tozo la ardhi na juhudi za kuomba msamaha lilianza tangu kipindi cha Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda na mawaziri wengine walihusishwa katika suala hilo.
“Chuo hakina hela, sijui watatunyang’anya wenyewe” alisema Pia alisema kuna College tatu ambazozina uhaba wa majengo na kuitaka serikali ikiangalie kwa jicho la huruma ili waweze kuondokana na changamoto hizo.
Akizungumzia kuhusiana na masuala hayo rais Magufuli alisema amepoka changamoto hizo na atazifanyia kazi. Alisema kama isingekuwa tume wa vyuo vikuu kupangiwa wanafunzi vyuo azma ya serikali ya Chuo Kikuu cha Dodoma kufikisha wanafunzi 40,000 ingefanikiwa.
“Ndio maana tumesema wanafunzi wachague pa kwenda sio wanakwenda kupangwa kwenye chuo kisicho na jina hakina hata nyumba za kukaa wakati hapa kuna mabweni mazuri kabisa” alisema Alisema majengo ya chuo hicho ni ya serikali na haoni ajabu kwa wizara za serikali kutumia majengo yake.
“Tulishasema tutahamia Dodoma na tumehamia hatutajali tunakwenda kukaa wapi” alisema Rais Magufuli. Alisema wakati Serikali kitangaza Dodoma kuwa makao makuu ya nchi mwaka 1973 alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la sita.
“Mpaka nikamaliza shule nikaenda chuo, nikawa waziri na sasa ni Rais lazima tuhamie Dodoma na tumeshahamia” alisema huku akishangiliwa. Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana alisema kama kuna mtu anasema Chuo kikuu cha Dodoma kina matatizo ana majungu.
Alisema mkoa unaendelea na utaratibu maalumu kwa ajili ya wanavyuo ambao ni wataalam wa barabara , afya na ualimu. “Tunafanya utaratibu ili washiriki kwenye kazi za aina mbalimbali wapate chochote ili wasisumbue kwenye hela za mkopo” alisema.
Spika wa Bunge Job Ndugai alisema Profesa Kikula ni miongoni mwa watanzania waliofanya mambo makubwa. “Serikali ifikirie kumpatia nishani ya aina yake amekuwa na malengo makubwa na chuo hiki tangu kinaanzishwa.” alisema

Tupia Comments: