SABABU za dawa za kiuavijasumu (antibiotics) kutokutibu wagonjwa ambao wanapata maambukizi ya vimelea mbalimbali zimefahamika. Sababu hizo ni pamoja na baadhi ya wagonjwa kushinikiza madaktari kuwaandikia dawa wanazotaka wao ambazo ni kiuavijasumu wakiamini kuwa zitawatibu wakati huo huo madaktari nao kulazimika kumuandikia dawa hizo ili aonekane anatibu vizuri na pia kumridhisha mgonjwa.
Wagonjwa ambao wanatumia dawa hizo kwa ugonjwa ambao haulazimiki kutibiwa kwa dawa hizo hujenga mazoea katika mwili wa mtu hivyo atakapopata ugonjwa ambao atatakiwa kutibiwa na dawa hiyo inashindwa kumtibu.
Aidha imebainika pia kuwa kiwango kidogo ambacho watu wanakila kutoka kwenye mimea na mifugo nacho hujenga usugu wa dawa hiyo, hivyo atakapohitajika kutumia dawa husika ili imtibu inakuwa imeshajenga usugu.
Imebainika pia kuwa baadhi ya mafamasia kutoa dawa bila mgonjwa kuwa na cheti cha daktari ambacho ameandikiwa dawa husika ni chanzo kingine cha tatizo la usugu wa dawa kwa binadamu.
Tatizo jingine ni kiwango ambacho binadamu wanakila kupitia mifugo yaani kwa kula nyama au kunywa maziwa ambayo hupatikana kwa mnyama au ndege aliyelishwa dawa za kiuavijasumu kwenye dawa kama tiba au vyakula wanavyokula.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mpango mkakati wa kitaifa wa miaka mitano kwa ajili ya kupambana na tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya.
Akizindua mpango huo juzi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mpoki Ulisubisya alisema kwa sababu ya matumizi ya dawa ambayo hayafuati imesebabisha vimelea ambavyo vilikuwa vinaweza kutibiwa kirahisi kwa aina moja ya dawa ya kiuavijasumu kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya usugu uliotokana na kutokunywa dozi sahihi.
“Vidudu hivyo kwa kutokupata tiba sahihi vinaanza kukua na kutengeneza usugu, tukipata ugonjwa ambao unatokana na vimelea vile vilivyotengeneza usugu dawa tulizonazo hazitaweza kutibu vile vidudu lakini mpango huu utasaidia kuelimishana na kuweka mipango mbalimbali kukabili tatizo,” alisema.
Katika tafiti zilizofanywa, asilimia mpaka 25 ya watoto ambao walipata vimelea hivyo na kutengeneza usugu walipoteza maisha huku zaidi ya watoto asilimia 70 wana usugu wa dawa za viuajisumu ambazo awali zilikuwa zikiwatibu.
Mpango huo utasaidia kutoa elimu kupitia njia mbalimbali, kuongeza uelewa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya, kupunguza matumizi ya kiuavijasumu kwa wanyama na watu, kupunguza tatizo, kuongeza njia za uwekezaji katika chanjo, tiba na dawa na pia mpango huo utaonesha maeneo ya vipaumbele na namna ya utekelezaji wake katika kila lengo.
Kwa nyakati tofauti wataalamu wa afya wametoa wito kwa mafamasia kutoa dawa hasa kiuavijasumu kwa wateja wao kwa kufuata maadili ya kazi zao. Walisema kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza tatizo la wananchi kutumia dawa kiholela bila maelekezo ya daktari jambo ambalo litaondoa pia tatizo la usugu wa dawa ambalo kwa sasa ni tatizo kubwa duniani.
Mganga Mkuu wa serikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Mohammed Bakari kwa utaratibu wa kawaida. Alisema ingawa hapa nchini mpaka sasa hali bado sio mbaya lakini lazima kudhibiti tatizo hilo kwani dawa zilizokuwa zikitibu miaka ya nyuma kwa sasa hazitibu tena na hiyo ni kutokana na usugu.
Mtaalamu mwingine kutoka shirika la HPSS, Profesa Manoris Meshack amesema zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanashinikiza madaktari kuwaandikia kiuavijasumu wakiamini kwamba ndio dawa ambazo zitatibu magonjwa yao. Alisema madaktari pamoja na wagonjwa wanachangia katika tatizo hilo la usugu wa dawa ambalo ni hatari kwa afya za watu.

Tupia Comments: