JESHI la Polisi Zanzibar limelazimika kufunga vituo vidogo katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kutokana kukabiliwa na upungufu wa askari visiwani hapo.


Akizungumza na Nipashe Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, alisema vituo hivyo vimefungwa na sasa vitalazimika kutumiwa na askari Jamii katika kuimarisha ulinzi.



“Tuna askari wachache ndiyo maana vituo vidogo tumelazimika kuvifunga na badala yake vitatumiwa na askari Jamii kutoa huduma za ulinzi katika maeneo yao.” alisema Kamishna Hamdan.



Alisema baada ya vituo hivyo kufungwa, wananchi wanatakiwa kuripoti matatizo yao katika vituo vya polisi vya karibu yakiwamo makosa ya uhalifu yanayotokea katika maeneo yao.



Hata hivyo, alisema ulinzi shirikishi wa polisi jamii bado haujahamasishwa kwa kiwango kikubwa Zanzibar licha ya hatua mbalimbali za viongozi wa polisi wilaya na mkoa kuchukua hatua za kuhamasisha wananchi.



“Bado ulinzi shirikishi wa polisi jamii haujahamasika pamoja na jitihada tunazochukua za kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wake,” alisema Kamishna huyo.



Kamishna huyo aliwataka wananchi kushirikiana na polisi katika kupambana na matukio ya uhalifu, ikiwamo kuendelea kuwafichua watu wanaoingiza na kuuza dawa za kulevya Zanzibar.



Alisema zoezi la kuwatafuta waingizaji na wauuza dawa za kulevya Zanzibar limepata mafanikio makubwa kutokana na kuadimika kwa watu wanaokutwa na dawa hizo.



Vituo vidogo vya polisi vilivyofungwa Zanzibar vilijengwa chini ya mpango wa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Augustino Mrema, ukiwa mkakati wake wa kupambana na uhalifu Zanzibar na Tanzania Bara.



Wakati huo huo, Kamishna Hamdan alisema kikosi cha doria katika sekta ya utalii kinaendelea kuimarisha ulinzi kuhakikisha ulinzi na usalama unaendelea kuwapo wakati huu wa kuelekea msimu wa utalii Zanzibar.

Tupia Comments: