Türkei Referendum | (picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis)
Chama kikuu cha upizani nchini Uturuki kimeitaka tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya kura maoni ya kihistoria nchini humo ambayo imempa madaraka mapya makubwa kabisa rais wa taifa hilo kutokana na ukiukaji mkubwa sana wa taratibu za kupiga kura.
Ujumbe wa kimataifa wa waangalizi ambao umeangalia kura hiyo ya maoni pia umegunduwa kuwepo kwa ukiukaji wa taratibu za kupiga kura kwa kusema upigaji kura huo hapo Jumapili ulikuwa haukukidhi viwango vya kimataifa.Hususan umekosowa uamuzi wa tume ya uchaguzi ya Uturuki kuzikubali kura ambazo zilikuwa hazina mihuri rasmi jambo mbalo imesema limedhoofisha usalama dhidi ya udanganyifu.
Tume hiyo ya uchaguzi ya Uturuki imethibitisha ushindi wa kura ya ndio katika kura hiyo ya maoni na kusema matokeo ya mwisho yataamuliwa katika kipindi cha siku 11 hadi siku 12 hivi.Shirika la habari la taifa Anadolu limesema kura za "ndio"  zilikuwa asilimia 51.4 wakati zile za "hapana" zilikuwa asilimia 48.6 .
Tafauti hiyo ya kura itaimarisha hatamu ya Erdogan madarakani nchini Uturuki kwa muongo mzima na inatazamiwa kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa kisiasa wa muda mrefu wa nchi hiyo na mahusiano yake ya kimataifa. Wapinzani wa mabadiliko hayo ya katiba hoja yao ilikuwa mageuzi hayo yanampa madaraka makubwa mno mtu ambaye amekuwa akizidi kuonyesha tabia za udikteta.
Alilazimika kupambana na mataifa yenye nguvu
Türkei Referendum Recep Tayyip Erdogan (picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis)
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Howard Eissenstat profesa mshiriki wa historia ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha St.Lawrence huko Canton,New York amesema "anatuhumu matokeo hayo ni finyu kuliko vile alivyokuwa ametegemea Erdogan".Ameongeza kusema " Erdogan aliwahi kutawala kwa ushindi wa kura chache hapo kabla na kwamba haoni ushindi wa kura chache kuwa ni kitu kengine ziada ya mamlaka.Msimamo wake emekuwa kutoujumuisha upinzani bali kuutokomeza".
Hapo Jumatatu Erdogan amewashambulia wakosoaji wake wa ndani na nje ya nchi kwa kusema "amelazimika kupambana na mataifa yenye nguvu duniani ambayo yalipinga kura ya ndio katika kura hiyo ya maoni ya kumuongezea madaraka."
Akihutubia wafuasi wake katika uwanja wa ndege wa Ankara hapo Jumatatu alipokuwa amewasili kutoka Istanbul amesema alikuwa "ameshambuliwa na mataifa yenye " mawazo "ya vita vya kidini dhidi ya Uislamu."
Haiko wazi iwapo alikukuwa akiyakusudia mataifa ya Ulaya yakiwemo Ujerumani na Uholanzi ambayo yaliwazuwiya mawaziri wake kufanya kampeni za mikutano ya hadhara kuwashawishi Waturuki wanaoishi katika nchi hizo kupiga kura ya ndio wakati wa kura hiyo ya maoni.
Merkel ataka serikali izungumze na upinzani
Merkel und Hollande Symbolbild (Getty Images/S. Gallup)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa .
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameitolea wito serikali ya Uturuki kufanya mazungumzo ya kina na vyama vyote vya kisiasa pamoja na asasi za kiraia, kutokana na ushindi finyu wa kura hiyo ya maoni kuonesha namna taifa hilo lilivyogawika. Katika taarifa ya pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sigmar Gabriel, Merkel amesema Ujerumani inaheshimu uamuzi wa watu wa Uturuki juu ya katiba yao, lakini wakati huo huo wamemtaka Rais Erdogan kutambua dhamana kubwa aliyonayo katika kuivuusha nchi yake kwenye hatua ya pili.
Ufaransa nayo imejiunga na Ujerumani kumtaka Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki kufanya mazungumzo na wapinzani wake wa kisiasa, kufuatia ushindi huo finyu sana kwenye kura ya maoni.  Rais Francoise Hollande wa Ufaransa amesema kwenye taarifa yake Jumatatu, kwamba ni juu ya Waturuki wenyewe kuamua utaratibu wa kisiasa, lakini matokeo ya kura hiyo ya maoni yanaakisi namna taifa hilo lilivyogawika.Lakini ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema maamuzi ya kura hiyo ni jambo la ndani na Uturuki, na kwamba lazima yaheshimiwe.
Tayari vyama vya upinzani vimesema vinakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo, ambayo yanampa madaraka makubwa kabisa Rais Erdogan.

Tupia Comments: