Baada ya kutumikia jeshi la Uganda (UPDF) kwa zaidi ya miaka 36 wanajeshi wote wakongwe wanastaafishwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana.
Hata hivyo serikali haijatoa sababu maalum ya uamuzi huo wa kuwastaafisha wanajeshi hao ambao wanajulikana kwa ushujaa wao wa kupigana vita vilivyomwezesha Rais Yoweri Museveni kuingia madarakani mwaka 1986.
Lakini kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi hilo Brigedia Richard Karemire hiyo ni hatua ya kawaida.
“Tutakuwa na uwezo wa kuwastaafisha zaidi ya maafisa 2000, wakiwemo majenerali,” amesema msemaji huyo.
Ameongeza kusema kuwa: “Tunalenga kuwastaafisha wanajeshi zaidi ya 2000 wakiwemo majenerali na zaidi ya wanajeshi wengine 10,000 watastaafu.”
“Hii ni sehemu ya zoezi ambalo limekuwa likiendelea kwa miaka mingi. Tunalenga kuimarisha utendaji kazi wa jeshi letu, kwani huko nyuma tayari tumewastaafisha baadhi yao,” amesema Brig Karemire.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa baadhi ya wanajeshi hawa wamekuwa wakitaka kuondoka jeshini bila ya mafanikio.
Ametoa mfano wa Generali David Tinyefuza ambaye tayari amefungua kesi ilioendelea katika mahakama nchini Uganda kwa muda wa miaka 8 akidai haki yake ya kustaafu bila ya mafanikio.
Kwa upande mwengine kumekuwa na baadhi ya wachambuzi ambao wamekuwa na maoni kuwa kulazimishwa kwa wanajeshi hao kubakia jeshini kunatokana na hofu kwamba wakiruhusiwa kustaafu wanaweza kujiingiza katika siasa na kuuporomosha utawala wa Museveni.
Mmoja wa wakongwe hao Jeshini Brigedia Generali Kasirye Gwanga anasema: “ Ni hatua nzuri waruhusu vijana wachukue usukani. Nina umri wa miaka 65 sasa, nafanya nini katika jeshi, siwezi kukimbia na kushiriki katika vita.”
Wanajeshi hao wakongwe walishiriki katika vita vya mwaka 1980 na 1985 pamoja na Rais Museveni dhidi ya utawala wake Apolo Milton Obote na Jenerali Tito Okello na kufanikiwa kumwezesha Museveni kuingia madarakani mwaka 1986 kwa mtutu wa bunduki.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda
Tupia Comments: